Friday, June 28, 2013

AMANA SHOOTING MABINGWA AIRTEL RISING STARS

Nahodha wa Amana Shooting, Abdul Mussa akipokea kombe la ubingwa wa irtel Rising Stars mkoa wa Ilala kutoka kwa mwenyekiti wa chama cha soka Ilala, Emmanuel Kazimoto huku ofisa wa IDYOSSA, Hugo Seseme (katikati) akishuhudia kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam jana.
 
Mshambuliaji  wa Amana Shooting Juma Kizairo akiwania mpira wa juu dhidi ya mchezaji wa  Buguruni Youth Center, Edward Jonas wakati wa mashindano ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars mkoa wa Ilala kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam jana. Amana Shooting ilishinda 1-0.


Mshambuliaji wa Amana Shooting, Juma Kizairo akichanja mbuga kuelekea golini wakati wa mashindano ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars mkoa wa Ilala kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam jana. Amana Shooting ilishinda 1-0.

Timu ya Amana Shooting imetwaa taji la ubingwa wa mkoa wa Ilala katika mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya Airtel Rising Stars baada ya kuifunga Buguruni Youth Centre 1-0 katika mchezo wa mwisho uliofanyika katika uwanja wa kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam, Alhamisi Juni 27.

Gori la pekee la Amana Shooting liliwekwa wavuni na mshambuliaji hatari Issaka Majaliwa dakika ya 32 baada ya ya kuwalamba chenga mabeki wa Buguruni Youth Center na kufunga kirahisi na kumuacha kipa Omari Hamisi akiduwaa. Hamisi Majaliwa alionyesha kipaji cha aina yake baada kuifungia timu yake magoli yote matatu iliyofunga katika mashindano hayo ngazi ya mkoa.

“Tumekiona kipaji cha huyu kijana na naamini atakuja kuwa mchezaji mzuri akiendelea kucheza kwa juhudi,” alisema katibu mkuu wa chama cha mpira wa miguu Ilala, Kanuti Daudi wakati akiongea na waandishi wa habari baada ya mchezo huo kumalizika.

Daudi alitamba kwamba kwa vipaji walivyonavyo mwaka huu timu ya Ilala kombaini ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Airtel Rising Stars ngazi ya taifa

Katika jiji la Mwanza, timu ya Alliance Schools Academy aliweka hai matumaini yake ya kutwaa kombe la ubingwa wa Airtel Rising Stars ngazi ya mkoa baada ya kuibugiza timu ya Nyamagana United 4-0 katika uwanja wa Nyamagana. 

Katika mchezo huo mshambuliaji hodari Athanas Adam ndiye aliyeng’ara vilivyo akifunga ‘hat trick’ kabla ya Kelvin Falu hajahitimisha karamu hiyo ya magoli dakika chache kabla ya mchezo kumalizika.  

Mashindano ya Airtel Rising Stars ngazi ya taifa yatashirikisha timu za wasichana na wavulana kutoka mikoa tisa – Kinondoni, Ilala, na Temeke itakayoleta timu za wasichana na wavulana wakati Tanga, Kigoma na Ruvuma zitashirikisha wasichana pekee huku mikoa ya Morogoro, Mwanza na  Mbeya ikiwa na timu za wavulana tu.

Maandalizi kwa ajili ya mtanange huo wa taifa yamekamilika na timu kutoka mikoani zinatarajiwa kuanza kuwasili jijini Dar es Salaam wikiendi hii tayari kwa mashindano hayo yatakayofanyika kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kuanzia Julai 2 hadi 7.

Fainali za ARS Taifa vile vile zilifanyika katika uwanja huo ambapo Temeke waliibuka washindi.

No comments:

Post a Comment