Thursday, April 11, 2013

WAKE WA MABALOZI WA NJE NCHINI KUMPIGA TAFU MISS TZ 2008 NASREEM KARIM

 
Mwenyekiti Msaidizi wa umoja wa wake wa mabalozi wa nchi mbalimbali duniani, Diplomatic Spouses Group (DSG), Keiko Okada (kulia) akizungumza jambo wakati akielezea nia yao ya kumsaidia Miss Tanzania 2008, Nasreem Karim (wa tatu kushoto) katika mpango wake wa kutengeneza mapambo kwa kutumia shanga za Kimasai.


Miss Tanzania 2008, Nasreem Karim (Katikati) akionyesha aina mbalimbali za mapambano ya shanga kwa ajili wa kuvaliwa na wanawake.
 

UMOJA wa wake wa mabalozi nchi mbalimbali duniani, Diplomatic Spouses Group (DSG), wameahidi kumpa msaada Miss Tanzania 2008, Nasreem Karim kupitia taasisi yake ijulikanayo kwa jina la Enjipai ambayo inajihusisha na uendelezaji na uhamasishaji wa kazi za mikono za wanawake wa Kimasai nchini.

Ahadi hiyo ilitolewa na mwenyekiti msaidizi wa DSG, Keiko Okada mara baada ya kuvutiwa na maonyesho ya Nasreem kuhusiana na mapambo mbali mbali ya wanawake yaliyotengezwa kwa kutumia shanga.

Mapambo hayo ni pamoja na mikufu, hereni, pete na vidani yametengenezwa kiustadi na mrembo huyo kwa kushirikiana na wanawake wa kabila hilo zaidi ya 20 wakiwa na lengo la kutangaza mila na desturi za kabila la Kimasai kupitia urembo.

Keiko ambaye ni mke wa Balozi wa Japani nchini alisema kuwa Nasreem ameonyesha kuwa ana nia ya kufanya hivyo na ni jukumu lao kumsaidia kama walivyofanya kwa vikundi mbalimbali hapa nchini.

“Ametuvutia sana, mradi wake ni mzuri na vifaa anavyotengeneza ni vizuri sana, ni mapambo mazuri kwa wanawake na kama unavyoona, baadhi ya wanawake wa mabalozi na wafanyakazi wa jumuiya za kimataifa wameanza kununua, hii imeonyesha ni jinsi gani alivyokuwa mbunifu katika fani hii,” alisema Keiko.

Alisema kuwa umoja wao una jumla ya wanachama zaidi ya 100 na wamesaidia vikundi mbalimbali ambavyo  vimeonyesha kufuata taratibu zao.

“Kwa Nasreem itakuwa rahisi zaidi kwani ameweza kufanya kazi hii bila msaada wowote kutoka nje, tutakaa na kuona anataka msaada wa aina gani,” alisema.

Nasreen alisema kuwa aliamua kuachana na kazi ya maonyesho ya mitindo nchini Afrika Kusini ili kuendeleza mila za Kimasai kwa kutengeneza mapambo mbali mbali kwa njia ya kisasa zaidi.

Alisema kuwa aliamua kuchagua kabila hilo hasa wanawake baada ya kugundua kuwa wanawake wa Kimasai wana uwezo wa kufanya kazi kwa muda mrefu na ni asili yao kufanya hivyo.

“Baada ya kufanikiwa kuwakusanya, nikaomba wanitajie neno la Kimasai lenye maana ya furaha, ndipo wakanitajia jina la Enjipai ambayo ndiyo taasisi yangu na kuizindua rasmi Desemba mwaka 2011, na tunaendelea vizuri licha ya changamoto mbalimbali,” alisema Nasreem.

Alisema kuwa moja ya changamoto kubwa ni kupata karakana ya kufanyia kazi zao za mikono, jambo ambalo wameshindwa kutokana na tatizo la kifedha.

No comments:

Post a Comment