Friday, April 5, 2013

MISS KIGAMBONI YAALIKA VIMWANA WAJITOKEZE KUSHIRIKI

KAMATI ya mashindano ya urembo ya kitongoji cha Kigamboni inawaomba warembo kutoka sehemu mbalimbali kujitokeza kuwania taji la shindano hilo litakalofanyika hivi karibuni.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, mratibu wa shindano hilo, wa kampuni ya K& L Media Solutions, Somoe Ng'itu, alisema kuwa nafasi iko wazi kwa wasichana wote wenye sifa za kushiriki shindano hilo kutoka sehemu mbalimbali nchini.

Mratibu huyo alisema kwamba lengo la kuweka wazi na kuwahamasisha warembo ni kutaka kutoa nafasi kwa wasichana wengi zaidi kujiandikisha na hatimaye kutoa ushindani kwenye kinyang'anyiro hicho kitakachofanyika baadaye mwezi ujao.

"Shindano letu liko wazi na tunakaribisha warembo kutoka sehemu yoyote hapa nchini kuchuana, tunataka mwaka huu tufanye vizuri zaidi katika mashindano ya Miss Tanzania," alisema Somoe.

Alisema kwamba kamati inaamini ushiriki mkubwa wa wasichana ndiyo utasaidia kutoa mshindi atakayeiwakilisha vyema Kigamboni katika mashindano yanayofuata ya Kanda ya Temeke na kwenye fainali za ngazi ya Taifa za Redd's Miss Tanzania. 

Aliongeza kuwa fomu kwa ajili ya shindano hilo zinatolewa bure na zinapatikana katika ofisi za gazeti la NIPASHE, Angella Msangi (TBC1), mgahawa wa Hadees ulioko Posta, ofisi za Miss Tanzania, na kwa barua pepe somoebaby@yahoo.com.

"Kigamboni ni eneo la kipekee na tunatarajia mwaka huu kufanya vizuri kwa kuwahusisha wadau wote kuanzia hatua ya kwanza hadi ya mwisho, tunafahamu mshindi ataiwakilisha Kigamboni na si kwamba ataenda kwenye fainali baada ya kupata ushirikiano wa wakazi wa eneo hili," aliongeza.

Mrembo anayeshikilia taji ni Edda Sylivester ambaye mwaka jana alishika nafasi ya tatu kwenye fainali za taifa huku mshindi wa taifa ni Brigitte Alfred ambaye mwaka huu ataenda kupeperusha bendera ya nchi katika mashindano ya dunia.

No comments:

Post a Comment