Saturday, April 13, 2013

MECHI ZA KURUSHWA 'LIVE' SUPERSPORT ZAYEYUKA


Mechi tano kati ya sita za Super Week za Ligi Kuu ya Vodacom zilizokuwa zioneshwe moja kwa moja (live) na Kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini sasa hazitaoneshwa kutokana na matatizo ya kiufundi.

Kwa mujibu wa Mtayarishaji Mtendaji (Executive Producer) wa SuperSport Kanda ya Afrika, Max Tshunungwa ambaye yuko nchini, wameshindwa kuonesha mechi hizo kutokana na matatizo ya kiufundi katika magari yao ya kurushia matangazo (OB van) yanayohudumia Afrika Mashariki- Kenya, Tanzania na Uganda.

Mechi hizo ni kati ya Azam na African Lyon, Yanga na Oljoro JKT, Azam na Simba, Coastal Union na JKT Ruvu na Mgambo Shooting na Yanga itakayochezwa Aprili 17 mwaka huu jijini Tanga.

Tatizo hilo pia limeathiri mechi za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) ambazo hazitaonekana wikiendi hii. SuperSport ndiyo yenye haki za matangazo ya televisheni kwa ligi hiyo ya Kenya.

Tshunungwa amekutana na Sekretarieti ya TFF na Kamati ya Ligi kuelezea tatizo hilo. SuperSport kwa kushirikiana na Kamati ya Ligi na TFF watapanga mechi nyingine za Super Week kabla ya ligi kumalizika msimu huu.

Pia TFF, Kamati ya Ligi na SuperSport watakuwa na mkutano mfupi wa waandishi wa habari wakati wa mapumziko kwenye mechi ya leo kati ya Yanga na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa.

No comments:

Post a Comment