Sunday, March 10, 2013

YANGA, TOTO MAPATO KIDUCHU


MAPATO ya mechi ya Yanga dhidi ya Toto Africans yamekuwa kiduchu zaidi ya yote kwa vinara hao wa ligi katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara msimu huu baada ya watazamaji 7,412 tu kuhudhuria kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Sh. 42,508,000 zilipatikana.

Mechi hiyo namba 135 iliyochezeshwa na Andrew Shamba kutoka mkoani Pwani ilimalizika kwa Yanga ambao wanaongoza VPL wakiwa na pointi 45 kuibuka na ushindi wa bao 1-0. Goli hilo lilifungwa na Nizar Khalfan. Mahasimu wao Simba, ambao mambo yao si mazuri, watajaribu kurekebisha hali ya hewa leo kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya Coastal Union ambayo iko katika kiwango cha juu.

Viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 9,406,764.95 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 6,484,271.19.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 6,708 na kuingiza sh. 33,540,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 89 na kuingiza sh. 1,780,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 4,783,100.82, tiketi sh. 4,136,390, gharama za mechi sh. 2,869,860.49, Kamati ya Ligi sh. 2,869,860.49, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,434,930.25 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,116,056.86.

No comments:

Post a Comment