Mrisho Ngassa (kulia) akijaribu kuwatoka wachezaji wa Coastal wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. |
Wachezaji
kibao wa kikosi cha pili cha Simba walionyesha kiwango cha juu na kufufua matumaini
yao ya kuikamata Azam baada ya kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Coastal Union
ya Tanga katika mechi yao kali ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam leo.
Kipa chaguo
la kwanza Juma Kaseja aliyeonekana jukwaani akiwa na mashabiki wengine wa kawaida, mabeki Juma Nyosso na Komalbil Keita, viungo Mwinyi
Kazimoto na Haruna Moshi 'Boban'; na straika wa kimataifa kutoka Zambia, Felix
Sunzu ni miongoni mwa nyota wa kikosi cha kwanza cha Simba walioachwa nje
katika siku ambayo taarifa zilishazagaa mitaani kuwa majina ya wakali kibao yalikabidhiwa
na uongozi kwa kocha Mfaransa Patrick Liewig wakidaiwa kuwa wanaihujumu timu na
hivyo aamue mwenyewe kuwapanga ama la.
Wakiongozwa
na Mrisho Ngassa, Nassoro Masoud 'Chollo' na Shomari Kapombe, kikosi kilichojaa
yosso cha Simba kiliwashangaza wengi kwa magoli mawili ya haraka katika dakika
tatu za majeruhi kabla ya mapumziko.
Ngassa
aliifungia Simba goli la kuongoza katika dakika ya 45 baada ya kuuwahi mpira
uliotemwa na kipa Shaaban Kado kufuatia shuti kali la Abdallah Seseme na Haruna
Chanongo akaongeza la pili muda mfupi kabla refa Martin Saanya hajapuliza
filimbi ya mapumziko.
Coastal
walikianza kwa kasi kipindi cha pili na walihitaji dakika nne tu kupata goli
lao kupitia Razak Khalfan aliyetumia vyema pasi ya Mohamed Athuman.
Tukio la
huzuni kwa Simba ni kuumia kwa Jonas Mkude aliyelazimika kutolewa uwanjani kwa
machela katika dakika ya 80 na nafasi yake kuchukuliwa na Mussa Mude.
Ushindi huo
ulimaanisha kwamba Simba waliocheza mechi 19 wamejihakikishia kubaki katika
nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 34, tatu juu ya Coastal,
Mtibwa na Kagera Sugar zilizocheza mechi 20 kila moja.
Yanga
inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 45, nane zaidi ya Azam iliyoshikiliwa kwa
sare na Polisi Morogoro jana huku kila moja ikishuka dimbani mara 19.
Vikosi:
Simba:- Abel
Dhaira, Nassoro Masoud 'Chollo', Miraji Adam, Hassan Khatib, Shomari Kapombe,
Jonas Mkude/Mussa Mude (dk. 80), Amri Kiemba, Rashid Ismail, Abdallah Seseme,
Haruna Chanongo na Mrisho Ngassa/Ramadhani Singano (dk. 73).
Coastal:-
Shaaban Kado, Hamad Hamis, Abdi Banda, Mbwana Hamis/Castory Mumbara, Philip
Mugenzi, Razak Khalfan, Daniel Lyanga, Mohamed Athumani, Deangelis da
Silva/Mohamed Mtindi (dk.75), Selemani Kassim Salembe na Joseph Mahundi/Twaha
Shekue (dk.46).
No comments:
Post a Comment