Saturday, March 30, 2013

MAITI ZILIZOCHOMOLEWA KATIKA MABAKI YA JENGO LA GHOROFA 16 LILILOPOROMOKA JANA JIJINI DAR ES SALAAM SASA ZAFIKIA 18... MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM SAID MECK SADICK ATHIBITISHA IDADI HIYO YA WAFU... ASKARI WA JKT WAMWAGWA KUSAIDIA KAZI NZITO YA KUCHOMOA WAHANGA WENGINE ZAIDI WALIONASA... MATUMAINI YAPUNGUA KUNASUA WALIO HAI... INAHOFIWA WATU KIBAO BADO WAMENASIA KWEYE KIFUSI...!

Mashuhuda wakiangalia jengo lililoporomoka asubuhi hii katika makutano ya Morogoro Road na Indira Gandhi jijini Dar es Salaam jana Machi 30, 2013.

 




Idadi rasmi ya watu waliokufa kufuatia ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 kwenye makutano ya Morogoro Road na Mtaa wa Indira Gandhi jijini Dar es Salaam imefikia 18 na inatarajiwa wengine zaidi watapatikana kutokana na shughuli za kunasua wahanga zaidi zinavyoendelea.

Taarifa iliyothibitishwa na afisa wa ikulu aliyemkariri mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick imedai kuwa hadi sasa shughuli za kuchimbua kifusi cha mabaki ya jengo hilo zinaendelea kufanywa kwa ushirikiano wa vikosi mbalimbali vya uokoaji, wataalam na vifaa kutoka makampuni mbalimbali ya ujenzi na pia kwa msaada wa vijana kibao waliomwagwa kutoka ndani ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Tukio hilo lilitokea jana asubuhi katika mitaa ya Posta, jirani na msikiti wa Shia katika eneo la makutano ya Morogoro Road na Indira Gandhi.

Jana, viongozi mbalimbali wa serikali na makamanda wa Polisi katika kanda maalum ya Dar es Salaam walifika kuangalia mwenendo wa shughuli za uokoaji, miongoni mwao akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadick ameamuru kusimamishwa mara moja kwa ujenzi wa jengo jingine la ghorofa 16 linaloendelea jirani tu na eneo lilikoanguka jengo la leo na kutaka kwanza kufanyike kwa uchunguzi zaidi ili kujiridhisha kuwa hatua za kiusalama na ubora wa jengo hilo zimefuatwa ili kuepuka maafa mengine.

Akizungumza jana jioni kupitia kituo cha televisheni ya taifa (TBC1), Sadick alisema kuwa serikali imeamua kusimamisha jengo hilo baada ya kubaini kuwa linafanana kwa kila kitu na jengo lililoanguka leo, ikiwa ni pamoja na mmiliki wake na pia mkandarasi anayeendelea na ujenzi huo.

Mungu azilaze pema roho za marehemu...Innalillahi wa inna illaihi rajiuun!

No comments:

Post a Comment