Tuesday, March 19, 2013

EPIQ STARS YAELEKEA MTWARA JUMAMOSI HIIMuendelezo wa ziara ya wasanii walioshiriki shindano la kuimba la Epiq BSS inaendelea jumamosi hii ya tarehe 23 katika viwanja vya Umoja zamani ukijulikana kama Nangwanda Sijaona kwa kiingilio cha shilingi elfu 2000 tu.

Burudani hiyo ambayo itaenda sambamba na kuadhimisha mwaka mmoja tokea club ya Maisha kuzinduliwa Mtwara, itaanza saa sita kamili mchana.

Wasanii watakaotumbuiza ni Menina Atick, Nsami Nkwabi, Nshoma, Vincent, Husna Nassor, Geofrey Levis, Wababa Mtuka, Norman Severino pamoja na mshindi wa milioni hamsini, Walter Chillambo.

Pamoja na wasanii hao kutoka Epiq Stars, burudani pia itatolewa na Linah, Barnaba, Ben Paul, na Rich Mavoko.

Wasanii hao ambao tayari wameshafanya show kali Dodoma na Dar es Salaam, wataendeleza moto wao kwa wakazi wa Mtawara na baadaye kutoa burudani katika Club Maisha Mtwara.

Wakazi wa Mtwara pia watapata kumsikia kwa mara ya kwanza mshindi wa miilioni hamsini Walter Chillambo akitoa burudani ya wimbo wake unaofanya vizuri kwenye vituo vya redio, Siachi, pamoja na nyimbo zake nyingine mpya.

Wasanii wengine ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye ziara za Dodoma na Dar, Godfrey, Menina, Norman, Husna pamoja na Wababa pia wanatarajiwa kuwakonga wana Mtwara.

Akizungumzia ziara ya Mtwara, Afsa Biashara Mkuu wa Zantel, Sajid Khan alisema wameamua kuwapelekea burudani wana Mtawara pia ili kuonyesha kuwa Zantel haina mipaka katika biashara zake.

‘Mwaka jana shindano la Epiq BSS lilifika hadi Lindi kutafuta vipaji, na sasa tunakuja Mtwara kuwaletea burudani ili kuonyesha kuwa Zantel inawajali’ alisema Khan.

Nao wasanii watakaotoa burudani Mtwara, wamesema wakazi wa Mtwara wajitokeze kwa wingi katika viwanja vya Umoja kushuhudia burudani kali.

‘Wakazi wa Mtwara wajiandae kupata burudani kali kutoka kwa Epiq Stars, lakini pia wajiandae kusikia nyimbo mpya kutoka kwangu, Norman na Godfery’ alisema Walter, mshindi wa Epiq BSS.

No comments:

Post a Comment