MATUKIO YA KIPIGO KILE: Wachezaji wa Mtibwa Sugar wakishangilia baada ya kufunga goli lao la kwanza |
Kocha wa enzi hizo wa Yanga, Tom Saintfiet akishuhudia kipigo kwenye Uwanja wa Jamhuri |
Wachezaji wa Yanga na Mtibwa walipokuwa wakiingia uwanjani siku hiyo |
Wachezaji wa Mtibwa wakipita kuwapa mikono wachezaji wa Yanga kabla ya kuanza kwa mechi hiyo |
Kikosi cha Mtibwa kilichotoa kipigo cha kukumbukwa kwa Yanga |
Mashabiki wa Mtibwa wakifurahia siku hiyo. Je kesho mashabiki wa upande gani watakaofurahi hivi? |
VINARA wa ligi kuu ya Vodacom, Yanga kesho watajaribu kulipa kisasi cha kipigo cha aibu cha 3-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar ya Morogoro wakati timu hizo mbili zitakaporudiana katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mechi yao ya awali iliyofanyika Septemba 19, 2012 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Yanga walikumbana na kipigo hicho kisichotarajiwa kilichosababisha uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani umtimue kocha wao Mbelgiji Tom Saintfiet baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa siku 80 tu na kuiongoza kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).
Mtibwa waliweka rekodi nzuri dhidi ya miamba ya soka nchini katika mzunguko wa kwanza baada ya kuwafunga pia Simba 2-0 kwenye uwanja huo huo na kumfanya kipa nahodha wa timu ya taifa, Juma Kaseja kumwaga kilio na wakati fulani alikaribia kuzipiga na aliyekuwa mshambuliaji wao Emmanuel Okwi katika tukio lililoonekana kupagawishwa na kichapo.
Mwamuzi Ronald Swai kutoka Arusha ndiye atakayechezesha mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na upinzani mkali, kwani wakati Yanga ikiongoza ligi hiyo, wapinzani wao Mtibwa Sugar katika mechi iliyopita walilala mbele ya Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho katika msimamo wa ligi kwa sasa.
Polisi Morogoro itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro wakati Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Ruvu Shooting inayofundishwa na Charles Boniface Mkwasa.
Keshokutwa (Jumapili) kutakuwa na mechi mbili. Simba itaumana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku Tanzania Prisons ikiikabili Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Kikosi cha Yanga kilichopigwa 3-0 na Mtibwa kwenye Uwanja wa Jamhuri kilikuwa:
Ali Mustapha 'Barthez', Juma Abdul, Mbuyu Twite/ Didier Kavumbagu (dk.64), Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Athumani Idd 'Chuji', Frank Domayo/ Simon Msuva (dk.46), Haruna Niyonzima, Said Bahanunzi, Hamisi Kiiza na David Luhende/ Stephano Mwasika (dk.46).
Mtibwa:
Shaban Kado, Maliwa Ndeule, Issa Rashid, Dickson Mbeikya, Salvatory Ntebe, Shaban Nditi, Jamal Mnyate, Awadhi Juma, Hussein Javu, Shaban Kisiga na Vincent Barnabas/ Ally Mohammed (dk.63).
No comments:
Post a Comment