Friday, February 1, 2013

ODEMWINGIE AGEUKA KITUKO KWA KULAZIMISHA KUHAMIA QPR... MASTAA WAMCHEKA KWENYE TWITTER

Peter Odemwingie

WAKATI dirisha la usajili nchini England likielekea kufungwa jana usiku, kulikuwa na matukio kadhaa yaliyofanyika katika dakika za lala salama.

Kali kuliko zote ilikuwa ni tukio la mshambuliaji wa West Brom Albion, Mnigeria Peter Odemwingie kujaribu kulazimisha uhamisho wake wa kujiunga na QPR kwa kwenda kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyo katika uwanja wa Loftus Road bila ya ruhusa ya uongozi wa klabu yake.

Mnigeria huyo alijikuta akiwa ameganda kwenye ngazi za makao makuu ya QPR baada ya dirisha la uhamisho kufungwa huku dili lake la uhamisho lililotarajiwa kugharimu paundi milioni 3 likiwa limekwama. 

Muda mfupi baadaye tukio hilo la Odemwingie likawa kituko kinachojadiliwa na mastaa katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

Nyota wa Arsenal, Alex Oxlade-Chamberlain alielezea hofu yake kuhusu mshambuliaji huyo baada ya dili lake kukwama: "Odemwingie anahitaji mahala pa kujihifadhi usiku wa leo?"

Kiungo wa Swansea, Wayne Routledge aliuliza: "Sasa Peter Odemwingie akitoka pale anaenda wapi?" Miongoni mwa majibu ya Twitter aliyopata moja wapo lilisema "Kituo cha basi".

Winga wa Norwich, Robert Snodgrass naye alipiga dongo: "Huyo ndiyo Odemwingie....... anahamia anakotaka #deadlineday"

Mtangazaji wa Sky Sports, Hayley McQueen alisema alitania kwamba baada ya kukwama jaribio lake, Odemwingie alikuwa hana pa kwenda hivyo akaibuka nyumbani kwake (mtangazaji) na kugonga hodi lakini hata yeye aliamua kumtosa kama alivyotoswa katika alichokuwa akilazimisha. McQueen aliandika: "Mimi naishi umbali wa dakika 10 tu kutoka Loftus Road, nilisikia hodi mlangoni, Odemwingie pengine? Wala sikwenda kumfungulia, sikutaka anione nikiwa nimetinga pajama langu."

Nyota wa zamani wa Newcastle, Darren Huckerby alionekana kupata ufumbuzi wa tatizo hilo. Aliandika: "(Kocha wa QPR, Harry) Redknapp alionekana akizungumza na Odemwingie nyumba ya Range Rover yake, kijana hataweza tena kurejea West Brom hivyo atakuwa mtunza bustani wa Harry."

No comments:

Post a Comment