Wednesday, February 27, 2013

YANGA SASA NI KAMA TRENI LISOKUWA NA BREKI... YAIPIGA KAGERA SUGAR 1-0 NA KUJICHIMBIA KILELENI MWA MSIMAMO WA LIGI HUKU IKIIACHA SIMBA KWA POINTI 11, AZAM POINTI SITA... MDUNGUAJI LEO NI YULEYULE ALIYEIUA AZAM- MRWANDA HARUNA NIYONZIMA 'FABREGAS'...!

Haruna Niyonzima 'Fabregas' akimtoka mchezaji wa Kagera wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.. 
Yanga waliendeleza kasi yao kama ya treni lisokuwa na breki baada ya kiungo Haruna Niyonzima 'Fabregas' kufunga bao pekee lililowapa ushindi wa 1-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

Matokeo hayo yamewaweka 'Wanajangwani' katika nafasi nzuri ya kuelekea ubingwa baada ya kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi sita dhidi ya Azam wanaowafuatia katika nafasi ya pili.

Yanga wamefikisha pointi 42 baada ya kuteremka dimbani mara 18, wakifuatiwa na Azam waliocheza idadi hiyo pia ya mechi. Mabingwa watetezi, Simba, ambao walipata kipigo kisichotarajiwa cha bao 1-0 kutoka kwa Mtibwa Jumapili, wanaendelea 'kumbwelambwela' katika nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 34.

Niyonzima ambaye ndiye aliyefunga goli pekee pia lililowapa Yanga ushindi wa 1-0 wakati walipocheza dhidi ya Azam Jumamosi, alifanya juhudi binafsi kwa kuwatoka mabeki kadhaa wa Kagera na kutishia kutoa pasi kabla ya kugeuka na kupiga shuti lililomshinda kipa  Hannington na kujaa wavuni katika dakika ya 66.
  
Goli hilo liliibua shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki wa Yanga ambao tayari walishaanza kuingiwa na hofu kutokana na kiwango cha cha juu cha wapinzani wao kilichowapa 'jeuri' kutawala mechi hiyo katika kipindi cha pili.
Mshambuliaji wa kimataifa kutoka Burundi, Didier Kavumbagu aliikosesha Yanga kupata goli la utangulizi kwa njia ya penati katika dakika ya 45 baada ya shuti lake kupaa juu ya lango.

Mwamuzi Simon Mberwa aliamuru ipigwe penati hiyo baada ya kipa wa Kagera, Hannington kudaka mguu wa Kavumbagu wakati akijaribu kuokoa na kipa huyo alionyeshwa kadi ya njano kwa kosa la kujaribu kupinga adhabu hiyo na kutishia kutoka uwanjani kabla ya kurejeshwa na kocha wake Abdallah Kibaden.

Frank Domayo alipiga shuti kali katika dakika ya 49 lililompita kipa wa Kagera na kugonga mwamba kabla ya mpira kurejea uwanjani.

Kagera walionyesha soka safi na kulishambulia zaidi lango la Yanga katika kipindi cha pili lakini wenyeji walisimama imara na kuokoa hatari kadhaa.
  
Straika Said Bahanunzi alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumvuta jezi George Kavilla wa Kagera katika eneo la kati ya uwanja na Nadir 
Haroub 'Cannavaro' alionyeshwa pia kadi ya njano katika dakika ya 82 baada ya kumkwatua Paul Ngwai aliyekuwa anaelekea kufunga.

Wachezaji Nizar Khalfan na David Luhende wa Yanga walifanya jumla ya kadi zote za njano kwa klabu yao jana kufikia tano wakati walipoadhibiwa wakiwa nje ya uwanja kwa kosa lililoonekana kuwa ni kugomea maelekezo waliyopewa na refa wa mezani. Kadi hizo zilimaanisha kuwa 'Wanajngwani' wajiandae kutozwa faini ya Sh. 500,000 kwa mujibu wa kanuni za ligi kuu ya Bara kuhusiana na adhabu kwa timu inayopata kadi za idadi hiyo katika mechi moja.

Baada ya mechi kumalizika, mashabiki wa Yanga waliojawa na furaha waliliendea basi liliolowabeba wachezaji wao na kuimba huku wakiwapongeza kwa kuwataja majina na kushangilia kwa kupuliza 'vuvuzela'.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo jana, Ruvu Shooting waliwashikilia wenyeji Coastal Union kwa sare ya 0-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku bao pekee lililofungwa na Nahoda Bakari katika dakika ya 51 likiwapa Polisi Morogoro ushindi wa 1-0 dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Jamhuri na Mtibwa walishindwa kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani Morogoro.

No comments:

Post a Comment