Friday, February 1, 2013

TENGA ATEUA WANASHERIA KAMATI YA NIDHAMU

Leodegar Tenga

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ameteua watu wawili kuingia kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya nafasi mbili kuwa wazi kutokana na mjumbe mmoja kuteuliwa kuongoza kamati nyingine ya TFF na mwingine kufariki dunia.

Iddi Mtiginjollah, ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Nidhamu aliteuliwa tarehe 23 Desemba 2013 kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi ya TFF baada ya Shirikisho kufanya mabadiliko ya katiba yaliyotokana na maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA), wakati mjumbe mwingine wa Kamati ya Nidhamu, Shaaban Semlangwa alifariki dunia katikati ya mwaka uliopita.

Kutokana na nafasi hizo kuwa wazi, Rais amewateua wafuatao kuziba nafasi hizo:

1.      Jesse Mguto- alikuwa Hakimu Mkazi na kwa sasa ni mwanasheria na Wakili wa Mahakama Kuu. Ana Digrii ya Sheria

2.      Yohane Masala- Kwa sasa ni Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali (Principal State Attorney). Ana Digrii ya Kwanza nay a Pili ya Sheria na Digrii ya Pili katika masuala ya Amani na Haki (MA in Peace and Justice).

Rais Tenga ameeleza kuwa ana imani na uwezo wa watu hao na kwamba watafanya kazi yao kwa uadilifu ili Shirikisho liendelee kuboresha utawala bora.

No comments:

Post a Comment