Hili ndilo goli pekee la Libolo lililotinga langoni mwa Simba leo...! |
Goli hilo pekee la Libolo liliwekwa wavuni na Joao Martins katika dakika ya 24 baada ya kuunganisha vyema kwa kichwa krosi kali kutoka kwa Dario Cardoso.
Simba sasa watalazimika kushinda ugenini mjini Luanda, Angola ili kuepuka mwendelezo wa aibu ya kung'olewa mapema katika michuano ya Afrika kwa klabu za Tanzania katika miaka ya hivi karibuni, hasa pale zisipopangiwa na timu 'vibonde' kama za visiwa vya Comoro katika hatua za awali au kujitoa kwa wpainzani wao.
Jana, Azam walianza vyema katika michuano ya Kombe la Shirikisho kwa kuibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Al Nasr ya Sudan Kusini, taifa ambalo linakamata nafasi ya 202 katika orodha ya viwango vya ubora wa soka duniani vilivyotolewa juzi na FIFA.
KASHKASH
Licha ya kufunga goli hilo, Waangola walioonyesha kiwango cha juu katika muda mwingi wa mechi na kuwapelekesha Simba mara kadhaa walikaribia kupata goli la pili katika dakika ya 44 wakati Gamaliel Mussumari alipopiga shuti kali lakini kipa Juma Kaseja alidaka kiufundi na kuibania Libolo, timu yenye jina baya kwa mtazamo wa lugha ya Kiswahili.
Winga Mrisho Ngassa alijaribu kufunga dhidi ya Libolo katika dakika ya 52 lakini beki wa wageni, Pedro Ribeiro aliokoa hatari hiyo.
Amri Kiemba alipiga pembeni katika dakika ya 65 na kupoteza nafasi ya kusawazisha baada ya kupokea pasi ya Haruna Moshi 'Boban' na beki Juma Nyosso aliyepanda mbele kusaidia mashambulizi alipiga shuti juu ya lango la Libolo akiwa ndani ya 18.
Mlindamlango wa Libolo, Landu Mavanga alidaka shuti la Kapombe na kuwanyima Simba goli la kusawazisha katika dakika ya 85, ikiwa ni dakika moja tu tangu mashabiki wa klabu hiyo ya Msimbazi kuzomea maamuzi ya kocha Mfaransa Patrick Liewig ya kumpumzisha Boban na nafasi yake kuingia Salim Kinje.
Baada ya mechi hiyo, kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu 'Julio' alisema kufungwa nyumbani hakumaanishi kwamba wameshatolewa na kwamba bado wana nafasi ya kubadili matokeo na kusonga mbele.
Vikosi vilikuwa;
Simba: Juma Kaseja, Nassor Masoud 'Cholo', Shomary Kapombe, Komalbil Keita, Juma Nyosso, Mussa Mude/ Amir Maftah (dk.53), Mrisho Ngassa, Amri Kiemba, Haruna Mosi 'Boban'/ Salim Kinje (dk.84), Mwinyi Kazimoto na Haruna Chanongo/ Ramadhani Singano 'Messi' (dk.66).
Libolo: Landu Mavanga, Carlos Almeida, Antonio Cassule, Pedro Ribeiro, Gamaliel Mussumari, Manuel Lopes, Sidnei Mariano, Dorivaldo Dias, Joao Martins/ Andre Madrid (dk. 70), Dario Cardoso/ Nuno Silva (dk.83) na Maieco Antonio/ Henry Camara (dk. 70).
No comments:
Post a Comment