Tuesday, February 26, 2013

REFA ALIYEVURUNDA MECHI YA SIMBA NA YANGA AFYEKWA JUMLA LIGI KUU BARA..!

Mathew Akrama

Mathew Akrama akimlima kadi nyekundu Simon Msuva wa Yanga katika mechi dhidi ya Simba.
Refa Mathew Akrama aliyechezesha chini ya kiwango mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyozikutanisha klabu zenye uhasama wa jadi za Simba na Yanga ameondolewa kuchezesha tena ligi hiyo msimu huu, imefahamika.

Akrama na marefa wenzake mbalimbali waliobainika kuwa 'wamechemsha' katika mechi mbalimbali za ligi hiyo wamechukuliwa hatua kadhaa za kinidhamu baada ya kupata alama za chini.

Refa Msaidizi wa FIFA, Ferdinand Chacha ameondolewa pia kuchezesha mechi za ligi kuu ya Bara baada ya kupata alama za chini katika mechi aliyochezesha kati ya African Lyon na Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Marefa wanaopata alama 6.5 au chini ya hapo kati ya 10 zinazohitajika ndiyo ambao hukumbwa na rungu kama lililomkuta Akrama na kuondolewa kwenye mechi za ligi kuu na pia za Ligi Daraja la Kwanza.

Marefa wengine walioondolewa kwa kutomudu mechi walizochezesha Ephrony Ndissa (Yanga vs Simba) na Ronald Swai (Yanga vs Mtibwa Sugar). 

Walioondolewa kwa kupata alama za chini ni Alex Mahagi (Simba vs JKT Ruvu), Methusela Musebula (Toto Africans vs Coastal Union), Lingstone Lwiza (Toto Africans vs Coastal Union), Idd Mikongoti (Toto Africans vs Mtibwa Sugar) na Samson Kobe (Toto Africans vs Mtibwa Sugar).

Masoud Mkelemi aliyekuwa refa wa mezani katika mechi ya FDL kati ya Moro United na Villa Squad ameondolewa kwa kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match meeting) na pia alichelewa kwa dakika tano kufika uwanjani.

MAKAMISHNA WASIMAMISHWA, WAONYWA
Baadhi ya makamishna wa ligi kuu na daraja la kwanza wameondolewa na wengine kusimamishwa kusimamia mechi za ligi hizo kutokana na upungufu kwenye ripoti zao au kutowasilisha kabisa ripoti hizo TFF baada ya mechi.

Kamishna Mohamed Jumbe aliyesimamia mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba ameondolewa kwenye orodha ya makamishna kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu.

Makamishna wa mechi kati ya JKT Oljoro vs Yanga (Hakim Byemba), JKT Oljoro vs Kagera Sugar (Salum Kikwamba), Toto Africans vs African Lyon (Charles Komba), Coastal Union vs JKT Oljoro (Mohamed Nyange) wamesimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao TFF.

Kwa upande wa FDL makamishna waliosimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao TFF ni wa mechi kati ya Kurugenzi vs Polisi Iringa, Morani vs Mwadui, Polisi Mara vs Pamba, Polisi Mara vs Mwadui, Morani vs JKT Kanembwa na Pamba vs Polisi Dodoma.

Wengine ni Mwadui vs JKT Kanembwa, Polisi Tabora vs Morani, Polisi Dodoma vs Polisi Mara, Polisi Tabora vs Mwadui, Polisi Mara vs Morani, JKT Kanembwa vs Polisi Mara, Morani vs Rhino Rangers na Small Kids vs Mkamba Rangers.

Kamati ya Ligi imewakumbusha makamishna wote kuwa ni jukumu lao kuhakikisha ripoti zao zimefika TFF na kurekebisha upungufu wa jinsi ya kuripoti matukio yanayotokea uwanjani. Licha ya kutuma nakala kwa njia ya email, wanatakiwa pia kuwasilisha ripoti halisi (original) TFF.

No comments:

Post a Comment