Tuesday, February 5, 2013

NJOONI KWA WINGI MZIONE STARS, CAMEROON


MENEJA wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambayo inadhamini timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, George Kavishe amewaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kesho Jumatano kuishangilia timu yao itakapocheza dhidi ya Cameroon katika mechi ya kirafiki.

Kavishe ameyasema hayo jijini Dar es Salaam na kusisitiza kuwa mechi hii ni  muhimu sana kwa Taifa Stars kujipima nguvu kwani Cameroon ni timu kubwa.

“Hii ni mechi kubwa sana kama ilivyokuwa ya Zambia mwaka jana na wote tulishuhudia timu yetu ikiibuka na ushindi,” alisema Kavishe.

Alisema wao kama wadhamini lengo lao ni kuona Stars inaendelea kufanya vizuri kwani timu hii imeshaonyesha uwezo mkubwa chini ya Kocha Kim Poulsen.

“Tangu tuanze kidhamini timu ya taifa tumeshuhudia mabadiliko makubwa na ni matumaini yetu kuwa kiwango hiki kitaendelea kuboreka,” alisema na kuongeza kuwa Watanzania wanatakiwa kuiunga mkono timu yao ya Taifa.

Kilimanjaro Premium Lager imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 10 katika timu ya Taifa na huu ndio udhamini mkubwa kuliko wote ambao Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) imewahi kupata kutoka kwa kampuni yoyote.

No comments:

Post a Comment