Saturday, February 23, 2013

NIYONZIMA AIPAISHA YANGA... BARAFU ZA AZAM ZAYEYUKA TAIFA


GOLI pekee kutoka kwa kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima lilitosha kuipa Yanga ushindi wa pili mfululizo msimu huu dhidi ya Azam FC katika mechi ya kugombea uongozi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

Ushindi huo, unamaanisha kwamba Yanga ambayo katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza iliwalaza Azam 2-0, imejiimarisha kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 39, tatu juu ya Azam iliyo katika nafasi ya pili, na nane juu ya mahasimu wao Simba walio katika nafasi ya tatu. Yanga na Simba zina mechi moja-moja mkononi.

Niyonzima alifunga goli hilo zuri kwa shuti la nje ya 18 katika dakika ya 32 kufuatia kugongeana na "one-two" na Jerry Tegete. Mpira ulikuwa kwa Niyonzima akampasia Tegete, ambaye alitisha kama anafumua shuti, mabeki walipojaribu kumzuia, akamtengea Niyonzima ambaye alifumua shuti lililomshinda kipa Mwadini Ali.

John Bocco alidhani ameifungia Azam goli la kusawazisha kwa kichwa kutokana na mpira wa kona katika kipindi cha kwanza lakini mwamuzi alilikataa kwa maelezo kwamba alimsukuma kipa Ali Mustapha 'Barthez' kabla ya kufunga.

Katika kipindi cha pili, straika wa Yanga, Didier Kavumbagu, alifunga goli ambalo lilikataliwa na mwamuzi pia kwa kuwa alikuwa ameotea.

Simba itacheza mechi yake ya 18 kesho dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo itajaribu kulipa kisasi cha kufungwa 2-0 kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Kipigo hicho cha mji kasoro bahari kilizua kizaazaa ambapo kipa Juma Kaseja alikaribia kuzipiga na aliyekuwa mshambuliaji wao Emmanuel Okwi, na baadaye katika tukio la kukumbukwa la baada ya mechi, Kaseja alimwaga kilio.

Kwenye uwanja huo wa Morogoro, Mtibwa pia iliisambaratisha Yanga kwa magoli 3-0 hadi klabu hiyo ya Jangwani ikamfukuza aliyekuwa kocha wake Mbelgiji Tom Saintfiet na kumleta wa sasa Mholanzi Ernie Brandts.

Yanga:
Ali Mustapha 'Barthez', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Athumani Idd 'Chuji', Simon Msuva, Frank Domayo, Jerryson Tegete, Hamis Kiiza/ Said Bahanunzi, Haruna Niyonzima.

Azam:
Mwadini Ali, Michael Bolou, Waziri Salum, Joackins Atudo, David Mwantika, Ibrahim Mwaipopo, Salum Abubakar 'Salum Aboubakar 'Sure Boy', John Bocco 'Adebayor', Kipre Tchetche, Humphrey Mieno na Khamis Micha.

No comments:

Post a Comment