Noma kwenye lango la Cameroon... |
MECHI ya kirafiki ya kimataifa kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Cameroon (Indomitable Lions) lililochezwa jana (Februari 6 mwaka huu) na wenyeji Stars kuibuka na ushindi wa bao 1-0 limeingiza sh. 148,144,000.
Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 23,092 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 22,598,237.29, maandalizi ya mchezo sh. 58,000,000 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 7,340,900.
Nyingine ni bonasi kwa wachezaji wa Taifa Stars sh. 18,831,864.41, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 8,274,659.66, asilimia 15 ya uwanja sh. 6,205,994.75 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 2,068,664.92.
Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 24,823,978.98 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,241,199 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.
KILIMANJARO LAGER YAIPONGEZA STARS
Mbwana Samatta akimuacha mtu wakati wa mechi ya Stars dhidi ya Cameroon |
Goooo! Chezea Sama Goal wewe!!!? Samatta akishangilia goli lake dhidi ya Cameroon kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. |
Wadhamini wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Kilimanjaro Premium Lager wamesema wanarishishwa na kiwango cha timu hiyo kwa sasa huku wakiomba TFF iandae mechi nyingi za Stars za kirafiki hapa nyumbani.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe siku moja baada ya Stars kuicharaza Cameroon bao 1-0 katika mechi ya kirafiki iliyopigwa katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
“Kwa kweli tunafurahishwa na mafanikio ya timu hii tangu tuchukue udhamini mwezi Mei mwaka jana….tumeiangalia ikicheza ndani na nje na kwa kweli kikosi ni kizuri kwani kimewaletea Watanzania ushindi,” alisema.
Aliwapongeza Watanzania kwa kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao kama kauli mbiu ya Kilimanjaro Premium Lager inavyosema…"Sherekea kilicho chetu."
“Hawa walikuwa wanajulikana kama Simba wa Afrika lakini wameondoka wakiwa wamenyong’onyea baada ya kufungwa 1-0,” alisema.
Kavishe alisema ushindi huu wa Stars umewapa nafasi nzuri ya kuendelea kuidhamini Taifa Stars ili kuwapa Watanzania nafasi ya kusherekea kilicho chao kwa kupitia burudani ya mpira.
“Kadri Watanzania wanavyozidi kutuunga mkono kwa kunywa bia yetu ya Kilimanajaro Premium Lager ndiyo sisi tunazidi kupata fedha za kuidhamini timu na kuendelea kuwapa burudani ya mpira,” alisema Kavishe.
Alisisitiza kuwa TFF inatakiwa kuandaa mechi nyingi za kirafiki hapa nyumbani ili Watanzania wazidi kuiona timu yao ikicheza.
Huu ni ushindi mnono wa pili mfululizo kwa timu ya Taifa baada ya kuichapa Zambia 1-0 Desemba mwaka jana.
No comments:
Post a Comment