Thursday, February 7, 2013

MAWAKILI RUKSA RUFANI ZA UCHAGUZI TFF


WAOMBAJI uongozi kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) waliokata rufani kupinga kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho wanaruhusiwa kuwa na uwakilishi wa kisheria (legal representation) wakati wa kusikilizwa rufani zao.

Uamuzi wa kuruhusu mawakili kwenye usikilizaji wa rufani hizo mbele ya Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF inayoongozwa na Idd Mtiginjola ni kuhakikisha kila upande unapata haki.

Pia Kamati ya Uchaguzi ya TFF ambayo ndiyo iliyosaili waombaji uongozi, hivyo kuwa mlalamikiwa katika rufani hizo, nayo inaruhusiwa kuwa na Wakili wakati wa usikilizaji wa rufani hizo.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaengua waombaji kumi na mbili wa uongozi kwenye nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo utakaofanyika Februari 24 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa kutokidhi matakwa ya kikatiba. Uchaguzi wa TPL Board utafanyika Februari 22 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Waombaji hao waliochujwa ni Omari Mussa Nkwarulo aliyeomba kuwania urais na Michael Richard Wambura aliyejitosa katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Makamu wa Rais.

Wengine waliochujwa wakiomba kugombea nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Abdallah Hussein Musa, Mbasha Matutu, Charles Mugondo, Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja, Eliud Peter Mvella, Farid Nahdi, Omari Isack Abdulkadir na Shafii Kajuna Dauda.

Kwa upande wa uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu aliyechujwa ni Christopher Peter Lunkombe aliyekuwa akiomba nafasi ya ujumbe katika Kamati ya Uendeshaji.

Mwisho wa kukata rufani kwa waombaji uongozi walioenguliwa na wale walioweka pingamizi kwa wagombea na zikatupwa ni leo (Februari 7 mwaka huu) saa 10 kamili jioni.

No comments:

Post a Comment