Monday, January 14, 2013

TFF YAPONGEZA UONGOZI MPYA RUREFA


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Januari 10 mwaka huu.

Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, amesema ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa RUREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Rukwa.

Wambura alisema TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya RUREFA chini ya uenyekiti wa Blassy Kiondo aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo uliofanyika mjini Sumbawanga.

Alisema uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Rukwa kwa kuzingatia katiba ya RUREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.

"Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF," alisema Wambura.

Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Blassy Kiondo (Mwenyekiti), Gregory Seko (Katibu), John Maholani (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Ayoub Nyaulingo (Mwakilishi wa Klabu TFF) na Gloria Ndawa (Mweka Hazina). Nafasi nyingine zitajazwa katika uchaguzi mdogo.

No comments:

Post a Comment