Monday, January 7, 2013

MOURINHO AZOMEWA, CASILLAS ASHANGILIWA... CASILLAS KIBURI... AMKAUSHIA MOURINHO WAKATI AKIMPA MAELEKEZO

Kipa Iker Casillas (kulia) akimliwaza kipa mwenzake wa Real Madrid, Antonio Adan, baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu na refa Iglesias Villanueva wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Real Sociedad kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid, Hispania jana Januari 6, 2013.
We ongea weee, sikuangalii usoni..... kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho akimpa maelekezo Iker Casillas kabla hajaingia uwanjani baada ya refa Iglesias Villanueva kumtoa kwa kadi nyekundu kipa Antonio Adan wa Real Madrid wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Real Sociedad kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid, Hispania jana Januari 6, 2013.
Kitambaa baki nacho tu mwana... Iker Casillas akimwachia Ronaldo aendelee kukivaa kitamba na unahodha katika mechi yao dhidi ya Real Sociedad jana. Ronaldo alimpelekea kitambaa Casillas baada ya nahodha huyo wa kudumu kuingia kutokea benchi katika dakika ya 6 kufuatia kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kipa Antonio Adan.


MASHABIKI waliokuwapo kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu wakati majina ya vikosi yakitajwa kwa ajili ya mechi ya Real Madrid dhidi ya Real Sociedad walizomea wakati lilipotokea jina la kipa Antonio Adan kwenye 'skrini' kubwa ya uwanjani, wakampigia makofi Iker Casillas na kumzomea kocha wao Jose Mourinho.

Pungufu ya dakika 10 kabla ya kuanza kwa mechi theluthi ya uwanja wa Real ilikuwa bado haijajaa na mashabiki wa Madrid walionyesha sapoti yao kwa kipa Iker Casillas - ambaye aliwekwa benchi kwa mara ya mechi ya pili mfululizo ya ligi – na wakamshutumu kocha wao, Mourinho kwa kumuanzisha tena kipa chaguo la pili Adan.

Kila kitu kilibadilika dakika chache baada ya mechi kuanza. Adan alimuangusha ndani ya boksi mshambuliaji wa Mexico, Carlos Vela, katika dakika ya 6, akatolewa kwa kadi nyekundu na nafasi yake ikachukuliwa na Casillas, jambo lililoamsha shangwe kubwa uwanjani.

Casillas alitumia takriban dakika nne kuvaa 'gloves' zake kabla ya kuijngia uwanjani. Wakati wa muda huo, ambao ni mara yake ya kwanza kuingia akitokea benchi katika kipindi cha miaka 10, Mourinho alimpa kipa huyo malekezo. Casillas hakumuangalia usoni Mourinho hata mara moja wakati akipewa maelekezo hayo, na badala yake alielekeza macho yake kwenye dimba la Santiago Bernabéu.

Wakati Casillas akiingia uwanjani, kwa mara nyingine mashabiki walisimama kuonyesha heshima yao kwake, lakini hakuweza kuzuia penalti iliyopigwa na Xabi Prieto, iliyofanya matokeo yawe 1-1 baada ya straika Mfaransa Karim Benzema kuwafafungia wenyeji goli la kuongoza mapema katika dakika ya 2. Ronaldo alifunga magoli mengine mawili na Khedira (1) katika ushindi wa 4-3. Magoli yote matatu yalifungwa na Prieto, ambaye alishindwa kuifurahia 'hat- trick' yake dhidi ya Casillas kutokana na kupoteza pointi zote tatu.

No comments:

Post a Comment