Thursday, January 24, 2013

MICHU ASAINI MIAKA MINNE SWANSEA

Michu

STRAIKA Michu amesaini mkataba mpya wa miaka minne wa kuendelea kubaki katika klabu yake ya Swansea City.

Mhispania huyo ameishangaza Ligi Kuu ya England tangu aliposajiliwa kwa dau "mbuzi" la paundi milioni 2.2 katika kipindi kilichopita cha usajili akitokea Rayo Vallecano.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 amesaini mkataba utakaomfanya abaki Liberty Stadium hadi mwaka 2016.

"Yalikuwa maamuzi mepesi sana kwangu,'' alisema Michu. "Naishi maisha ya ndoto yangu hapa Swansea."

Michu, ambaye anaweza kucheza kama kiungo mshambuliaji au mshambuliaji wa kati, amefunga magoli 16 katika mechi 28 alizochezea Swans.

Tayari ametajwa kama ndiye usajili bora wa msimu na wachambuzi wa soka na amekuwa shujaa wa Swansea.

Kocha Michael Laudrup amesifu mchango wa straika wake huyo na amemuelezea kama ndiye mchezaji "dili zaidi msimu huu."   

"nimesikiliza uvumi wote uliotawala, lakini haukunisumbua na ndiyo maana nimesaini mkataba mpya," alisema.

Alianza kucheza soka katika klabu ya mjini kwao ya Real Oviedo katika ligi za chini, kabla ya kuhamia Celta de Vigo B katika Ligi Daraja la Pili ya Hispania (Segunda B) mwaka 2007.

Mkataba wake na Celta ulimalizika Juni 2011 na akasaini mkataba wa miaka miwili na Rayo Vallecano, ambao wamepanda daraja hadi La Liga msimu huu, ambako alifunga magoli 15 ya ligi na mawili katika Kombe la Mfalme msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment