Thursday, January 24, 2013

MESSI AZIDI KUWEKA REKODI LA LIGA... WACHEZAJI 69 WALITWAA TUZO YA "PICHICHI" KWA PUNGUFU YA MAGOLI 29 ALIYONAYO SASA

Messi akishikilia tuzo yake ya Kiatu cha Dhahabu 2012
Messi akishikilia tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia 2012

MAISHA ya soka ya Lionel Messi yanaendelea kuwa ya maajabu. Akiwa ndiyo kwanza ana umri wa miaka 25, bado hajafikia kilele chake na bado anaendelea kuchanja mbuga akiweka rekodi zake katika ulimwengu wa soka. Msimu huu tayari amefunga magoli 29 katika mechi 20 za La Liga alizocheza.

Messi yuko katika nafasi ya kuivunja rekodi yake mwenyewe aliyoiweka mwaka jana, ambayo ilikuwa ni kufunga magoli 50 ya La Liga, jumla ambayo ilimfanya ashinde tuzo ya 'Pichichi' ya mfungaji bora wa Ligi Kuu pamoja na tuzo ya Kiatu cha Dhahabu kwa takwimu bora zaidi za muda wote katika tuzo zote mbili. Kama ataendelea na wastani huu, anaweza kufikisha magoli 55 msimu huu katika ligi kuu.

Jumla ya magoli yake inatisha na inawafunika vibaya wafungaji bora wa historia ya La Liga. Kwa msimu huu pekee, anahitaji goli moja tu kufikia idadi ya asilimia 80 ya washindi wa tuzo ya Pichichi wa ufungaji bora wa ligi nzima wa miaka ya nyuma tangu ligi hiyo ilipoanzishwa. Au, kwa maneno mengine, ni kwamba kati ya washindi 88 wa tuzo ya Pichichi wa tangu msimu wa 1928-29, ni washindi 19 tu waliotwaa tuzo hiyo kwa kufunga zaidi ya magoli 28, ambayo Muargentina huyo tayari ameyapita msimu huu huku ligi ikiwa ndiyo kwanza bado "mbichi".

Messi, hata hivyo, ana mechi 18 za kuendelea kufunga. Kama atafunga Jumapili hii dhidi ya Osasuna, atawapiku wafungaji bora wengine wanne (Maakay, Bebeto, Hugo Sánchez na Krankl), ambao walitwaa tuzo ya Pichichi wakiwa na magoli 29.

No comments:

Post a Comment