Wednesday, January 9, 2013

GUARDIOLA ATAIFUNDISHA MAN CITY - STOICHKOV

Pep Guardiola
Hristo Stoichkov


NYOTA wa zamani wa Barcelona, Hristo Stoichkov, ambaye alicheza kikosi kimoja na Pep Guardiola klabuni Barca, anaamini kwamba kocha huyo atatua Manchester City siku moja.

Guardiola (41) amethibitisha juzi kwamba amedhamiria kurejea kufundisha soka katika msimu ujao wa 2013-14, na klabu kama Bayern Munich, Chelsea, Manchester City na Arsenal zote zinaaminika kumuwania.

"Namuona Guardiola akihamia Manchester City. Ushirikiano wa mkurugenzi wa ufundi Txiki Begiristain na kocha Pep Guardiola ulileta miujiza Barca," Stoichkov aliiambia Esports Cope.

Nyota huyo wa zamani wa Bulgaria kisha akamfagilia mshindi wa tuzo ya FIFA Ballon d'Or 2012, Lionel Messi, kufuatia kucheza kwa kiwango cha juu.

"Ni jambo kubwa sana kwa mchezaji kutwaa tuzo ya Ballon d'Or. Ni kazi ya watu wengi sana," alisema.

"Nina hakika kwamba Messi ataendelea kushinda tuzo ya Ballon d'Or kwa miaka mingine kadhaa, na hakika anastahili. Hapajatokea mchezaji mwenye kipaji na aliyekamilika kama yeye kwa miaka 10 iliyopita."

Aliongeza, "Na amezungukwa na wachezaji bora."

Messi amekuwa mchezaji wa kwanza katika historia kutwaa tuzo ya mwanasoka Bora wa Dunia mara nne mfululizo.

No comments:

Post a Comment