Wednesday, January 9, 2013

FABREGAS: NIKO KATIKA KIWANGO BORA KABISA CHA MAISHA YANGU

Fabregas

Cesc Fabregas wa Barcelona akiangushwa na kipa wa Espanyol, Kiko Casilla na kuzaa penalti iliyofungwa na Lionel Messi wakati wa mechi yao ya La Liga kwenye Uwanja wa Nou Camp mjini Barcelona, Hispania Jumapili Januari 6, 2013.

USHINDI wa Barcelona wa 4-0 dhidi ya Espanyol Jumapili ulishuhudia kurejea uwanjani kwa Cesc Fabregas aliyekuwa nje ya uwanja mwezi mzima kutokana na majeraha aliyoyapata katika mechi dhidi ya Real Betis.

Kiungo huyo wa ushambuliaji alijifua sana ili asiikose mechi ya wapinzani wa jadi wa jimbo la Catalunya dhidi ya Espanyol na Tito Vilanova aliamua kumuamini kwa kumpa nafasi ya kuwakabili majirani zao. Fabregas naye alilipa fadhila za kuaminiwa kwa kucheza kwa kiwango cha juu ikiwamo kusababisha penalti iliyofungwa na Lionel Messi.

Fabregas anaamini kwamba Vilanova ndiye nguzo ya mafanikio yake msimu huu, baada ya kocha huyo kumpa nafasi katika kipindi ambacho aliihitaji zaidi mwanzoni mwa msimu.

"Nilihitaji sapoti aliyonipa. Nilikuwa naenda uwanjani nikijisikia tofauti kabisa. Nilijiweka mwenyewe katika presha. Kulikuwa na uvumi umezagaa, lakini kocha aliniamini akanipanga kikosini na sasa nimetulia zaidi na najiamini. Niko katika kiwango bora zaidi cha maisha yangu. Hii ni tangu nilipofika hapa."

Kiungo huyo wa Barca alirejea uwanjani kama ilivyotarajiwa.

"Nilijisikia vyema sana na nikafanya kazi kwa bidii sana. Nilipoumia nilimweleza dokta nataka kupona ndani ya muda ili niiwahi mechi hii. Nilifanya kazi kwa bidii asubuhi na jioni hadi katika kipindi cha mapumziko ya Krismasi ili kutimiza lengo lango. Nilikuwa na bahati kwa sababu kuumia kwangu kuliingiliana na mapumziko ya Krismasi hivyo ilinisaidia kujiandaa."

Fabregas pia alielezea furaha yake kutokana na kurejea kwa Vilanova kutokea kufanyiwa upasuaji: "Ilikuwa ni jambo kubwa timu kwa yeye kurejea mapema. Dhamira yake ya kutaka kurejea uwanjani itakuwa imemsaidia kupona haraka."

No comments:

Post a Comment