Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaupongeza uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika juzi (Desemba 12 mwaka huu) hoteli ya Mbezi Garden.
Ushindi aliopata Almasi Kasongo aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji unaonesha jinsi ambavyo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa DRFA walivyo na imani kwao.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya DRFA ambayo hivi sasa ina kinara mpya, na kwamba ina changamoto kubwa ya kuhakikisha inaendesha shughuli za DRFA kwa kuzingatia katiba na kanuni.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA chini ya Juma Simba na Kamati ya Uchaguzi ya TFF inayoongozwa na Deogratias Lyatto kwa kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia katiba na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Safu mpya ya uongozi wa DRFA inaundwa na Kasongo (Mwenyekiti), Meba Ramadhan (Makamu Mwenyekiti), Msanifu Kondo (Katibu), Muhsin Said (Mwakilishi wa Mkutano Mkuu wa TFF), Benny Kisaka (Mwakilishi wa Klabu), Ally Hobe (Mhazini) na wajumbe Mohamed Shabani, Sunday Mwanahewa na Bakari Mapande.
No comments:
Post a Comment