Thursday, December 27, 2012

JOE HART AKATAA KOMBE LISHAWAPONYOKA KWA MAN UNITED

Kipa wa Manchester City, Joe Hart (kushoto) akiliwazwa na Adam Johnson wa Sunderland baada ya mechi yao ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Stadium of Light mjini Sunderland, England jana Desemba 26, 2012. Man City ililala 1-0 kwa goli lililofungwa na winga huyo wa zamani wa City, Adam Johnson.

Kipa wa Manchester City, Joe Hart "akilamba mchanga" baada ya kufungwa goli lililowazamisha dhidi ya Sunderland wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Stadium of Light mjini Sunderland, England jana Desemba 26, 2012. Man City ililala 1-0.

KIPA wa Manchester City, Joe Hart anaamini kwamba mabingwa hao wa Ligi kuu ya England watatetea taji lao licha ya kuwa nyuma ya Manchester United kwa pointi saba baada ya kipigo chao cha 1-0 ugenini dhidi ya Sunderland.

Kocha wa Man City, Roberto Mancini haraka alisema kwamba msimu ndiyo kwanza uko nusu huku akisema kipigo hicho kisichotarajiwa kimewauma, na Hart anaamini ngoma bado mbichi.

Aliiamboa tovuti rasmi ya klabu hiyo: "Tuliwahi kuongoza, United waliwahi kuongoza ni kama kupokezana vijiti kwa sasa.

"Sisi ni timu ya ushindi. Ni ngumu na inauma, lakini ni lazima tusonge mbele. Ni vigumu kuongoza na ni vigumu kumfukuza anayeongoza pia."

No comments:

Post a Comment