Saturday, December 22, 2012

HATARI ...! KONTENA LILILOJAA KONDOM MIBOVU LANASWA BANDARINI DAR.... LIMESHEHENI KONDOM KUTOKA INDIA ZENYE MATUNDU KIBAO NA AMBAZO HUPASUKA KIRAHISI MNO... SHIRIKA LA VIWANGO TBS LADAI NYINGINE ZA AINA HIYO HIYO ZIMEKUTWA KWENYE MADUKA KADHAA YA DAWA JIJINI DAR ES SALAAM BAADA YA MIHUNI KUZISAMBAZA FASTA ... HOFU YA WATUMIAJI WAKE KUBEBA HIV YATANDA

Kontena  kubwa lililosheheni kondomu za kiume kutoka nchini India limekamatwa na kuzuiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam, baada ya kubainika kuwa kondom zilizomo hazifai kabisa kwa matumizi ya binadamu na kwamba pia haziwasaidii lolote watumiaji kujiepusha na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU a.ka HIV).

Maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wamelazimika kufanya msako mkali kwenye baadhi ya maduka ya dawa jijini Dar es Salaam na kupatwa na mshtuko baada ya kubaini kuwa tayari kondom hizo mbovu zipo sokoni na wananchi wanaendelea kuzitumia bila hofu kwani hakuna ajuaye kuwa ni mbovu na tena ni hatari kwa afya zao.


Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Leandri Kinabo, alizitaja kondomu hizo kuwa ni aina ya Melt Me zenye thamani ya Sh. milioni 222.1, ambazo zilikamatwa tangu Oktoba 23, 2012 na kuzuiliwa bandarini hapo kwa taratibu zaidi za kisheria.

“Jambo lililotushtua ni kwamba zimebainika zipo madukani, tukajaribu kufuatilia tena bandarini tukifikiri kuwa huenda zimetolewa kinyemela licha ya kuzuiliwa ili ziteketezwe au zirejeshwe nchini India kwa gharama zao wahusika.

Tulipokwenda bandarini tukabaini kwamba bado zipo katika hali ile ile, kumbe  zimeingizwa nchini kwa njia ya panya, kwa kweli ni mbovu na ndiyo maana tumelazimika kuwajulisha wanahabari ili muwape taarifa wananchi wawe makini,” alisema Kinabo.

Alifafanua zaidi kwamba kondomu hizo ni mbovu kwani zimebainika kuwa na vitundu, pia zinapasuka haraka, hazina kabisa viwango vya ubora wa bidhaa unaotakiwa na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO).

Kinabo alisema kuwa wao (TBS) bado wanaendelea kufanya mawasiliano na kampuni iliyotengeneza kondomu hizo.

Alisema kuwa katika kasha lake, inaonyesha kuwa kondom hizo 'feki' zinaingizwa nchini na kampuni ya Fair Deal Exim ya Dar es Salaam.
Kufuatia taarifa ya kuenea madukani kwa kondom hizo mbovu, tayari kumekuwa na hofu kubwa kwa watumiaji kupata maambukizi zaidi ya virusi vya HIV kwani baadhi yao wamekuwa wakijiamini kwa kinga hizo ambazo kumbe si lolote si chochote. Kazi ipo!

No comments:

Post a Comment