Monday, December 17, 2012

BARCA YAIPIGA ATLETICO 4-1, MESSI ATUPIA 2 AFIKISHA MABAO 90, REAL YASHIKWA 2-2, YAACHWA POINTI 13... MASHABIKI BARCA WAIMBA "MOURINHO TUNAKUPENDA, MOURINHO USIONDOKE"

Lionel Messi (kushoto) akishangilia pamoja na Puyol (kulia) na Xavi

Xabi Alonso (kushoto) wa Real Madrid akisikitika pamoja na Cristiano Ronaldo (katikati), Sergio Ramos na Iker Casillas (kulia) baada ya Espanyol kufunga goli lao la pili wakati wa mechi yao ya La Liga kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu jana usiku Desemba 16, 2012.
Cristiano Ronaldo (katikati) wa Real Madrid akilimwa kadi ya njano na refa Antonio Miguel baada ya kucheza rafu wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Espanyol kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu jana usiku Desemba 16, 2012.

Cristiano Ronaldo wa Real Madrid akishangilia goli lake dhidi ya kipa Francisco Casilla wa Espanyol kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu jana usiku Desemba 16, 2012.

Cristiano Ronaldo wa Real Madrid akishangilia goli lake dhidi ya kipa Francisco "Kiko" Casilla wa Espanyol kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu jana usiku Desemba 16, 2012.
Wapi rekodi ya Zico ya magoli 89?... Lionel Messi wa Barcelona akishangilia goli lake la 90 mwaka huu wakati wa mechi yao ya La Liga kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona Hispania jana usiku Desemba 16, 2012.
Lionel Messi (kulia) wa Barcelona akiubetua mpira kufunga goli la nne la timu yake pembeni ya Miranda wa Atletico de Madrid wakati wa mechi yao ya La Liga kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona Hispania jana usiku Desemba 16, 2012.

Lionel Messi (kulia) wa Barcelona akiubetua mpira juu ya kipa Thibaut Courtois wa Atletico de Madrid na kufunga goli lake la 90 mwaka huu wa 2012 wakati wa mechi yao ya La Liga kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona Hispania jana usiku Desemba 16, 2012.
Shabiki aliyevamia uwanjani akishangilia baada ya kumkumbatia Lionel Messi wa Barcelona wakati wa mechi yao ya La Liga kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona Hispania jana usiku Desemba 16, 2012.


Shabiki aliyevamia uwanjani akishangilia baada ya kumkumbatia Lionel Messi wa Barcelona wakati wa mechi yao ya La Liga kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona Hispania jana usiku Desemba 16, 2012.

LIONEL Messi alifunga magoli mawili na kutimiza mabao 90 mwaka huu wakati alipoisaidia Barcelona kuendeleza mwanzo mzuri wa msimu baada ya jana usiku kuifunga timu inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa La Liga ya Atletico Madrid kwa magoli 4-1 huku mahasimu wao Real Madrid wakishikiliwa katika sare ya kufadhaisha ya 2-2 nyumbani dhidi ya Espanyol.

Ushindi unamaanisha kwamba Barcelona imeipita Atletico kwa pointi 9 na imeiacha Real Madrid kwa pointi 13, jambo lililomfanya kocha wa Real, Jose Mourinho kusema kwamba mbio zao za ubingwa zimemalizika. 

Kulikuwa na mambo ambayo hayakuwahi kuonekana: Atletico kucheza soka zuri dhidi ya Barca katika kipindi cha kwanza, ambalo hata hivyo halikuwasaidia "mwisho wa siku". Pia mashabiki 100,000 wa Barcelona kwenye Uwanja wa Nou Camp kuimba kwa pamoja: "Mourinho tunakupenda, Mourinho baki".

Falcao 'The Tiger' aliwasili Camp Nou akiwa na dhamira ya kufunga. Nafasi yake ya kwanza langoni alipiga kichwa kilichogonga nguzo kwa ndani na mpira kusesereka mbele ya lango kabla ya kuokolewa, akapiga shuti nje baada ya kuanzishiwa 'fri-kiki' ya haraka kabla ya kufunga kiufundi katika jaribio lake la tatu baada ya kuwazidi mbio wachezaji wa Barca na kuudokoa juu ya kipa Victor Valdes. Huku wakiongoza 1-0 Atlético walithibitisha kwamba wanastahili kuongoza na kwamba walidhamiria kuwashangaza Barça.

Hata hivyo, beki Adriano alitokea kusikojulikana na kufunga bonge la bao kwa shuti la upinde wa mvua lililogonga besela kabla ya kutinga wavuni na kumfanya kipa mwenye urefu wa futi 6 na inchi 5, Thibaut Courtois, ambaye anaichezea Atletico kwa mkopo akitokea Chelsea, ashindwe kuuzuia. Goli hilo kali ni kama liliwachanganya Atlético na ushindani wao ulifikia tamati. Safu ya ulinzi ya wageni ilianza kufanya makosa mfululizo yaliyowapa Barça goli la pili, lililofungwa na Sergio Busquets, aliyeandika goli lake la kwanza msimu huu kutokana na mpira wa kona uliozagaa langoni.

Barça walienda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 2-1 huku Messi akiwa amebanwa na kuonekana kama shabiki wa kawaida tu uwanjani.

Kipindi cha pili, Messi alifunga goli la tatu la timu yake baada ya kuuburuza msitu wa mabeki waliokuwa wakimchunga na akaongeza la nne kufuatia makosa ya beki Diego Godín kutoa pasi ya kisigino iliyoibwa na Messi aliyefunga kwa kuudokoa mpira juu ya kipa aliyejaribu kulala chini na kuipa Barca ushindi wa 4-1.

Katika mechi iliyochezwa mapema jana, Real  Madrid ililazimishwa sare ya 2-2.

Sergio García aliwafungia Espanyol goli la kuongoza kabla ya Cristiano Ronaldo kufunga goli lake la 126 la ligi na Fabio Coentrao akaongeza la pili kuwafanya wenyeji waongoze 2-1. Hata hivyo zikiwa zimebaki dakika mbili, Albin mwenye rekodi nzuri ya kuifunga Real Madrid, aliifungia Espanyol goli la kusawazisha.

Mashabiki wa Real Madrid kwenye Uwanja wa Bernabeu waliendelea kuizomea timu yao na kocha Jose Mourinho kutokana na mwendo mbaya wa timu.

Real Madrid tayari imeshapoteza pointi nyingi msimu huu katika La Liga, 15 jumla, kuliko ilizopoteza msimu mzima uliopita ambapo walidondosha pointi 14 tu na kumaliza wakiwa na pointi 100.

Mambo hayako hivyo msimu huu kwani hata kama watashinda mechi zao zote 22 zilizobaki hawatafikisha pointi 100, wataishia pointi 99.

Real wametoka sare mara mbili nyumbani: dhidi ya Valencia (1-1) na Espanyol (2-2). Ugenini walilala kwa Getafe (2-1), Sevilla (1-0) na Betis (1-0).

No comments:

Post a Comment