Umony (mbele) akimuacha mtu wakati wa michuano ya Chalenji iliyoisha Jumamosi. |
KLABU ya Azam imezidi
kujiimarisha baada ya kumsajili straika wa kimataifa wa Uganda, Brian Umony kwa
dau lisilotajwa lakini linalodaiwa kuwa ni la ‘hela ndefu’ ya mamilioni ya
fedha, imefahamika.
Taarifa zilizothibitishwa leo na Meneja wa Azam, Patrick Kahemele, zimeeleza kwamba straika huyo bora wa Uganda ‘aliyefunika’ ile mbaya
katika michuano iliyomalizika hivi karibuni ya Kombe la Mataifa ya Afrika
Mashariki na Kati (Kombe la Chalenji) na kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa
Chalenji 2012, ameshamalizana na waajiri wake wapya na kusaini mkataba wa miaka
miwili.
Ataichezea timu hiyo katika
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Akizungumza leo kutokea Kampala,
Meneja wa Azam, Patrick Kahemele, alisema kuwa tayari wameshamalizana na Umony
na mchezaji huyo atatua jijini Dar es Salaam kesho kujiunga na wachezaji
wenzake walio kambini kujiandaa na ziara yao ya Kinshasa nchini Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo.
“Kila kitu kimeshakamilika,
tumeshaingia naye (Umony) mkataba wa miaka miwili na kesho kutwa atapanda ndege hapa Kampala kuja huko (Dar es
Salaam) kuungana na wachezaji wenzake wa Azam,” amesema Kahemele, ambaye hata
hivyo hakuwa tayari kutaja ada ya uhamisho waliyotumia kumpata mchezaji huyo
wala maslahi yake.
Afisa Habari wa Azam, Jaffer Idd
Maganga, alisema kikosi chao kitaondoka jijini Dar es Salaam Ijumaa kuelekea
Kinshasa ambako kitaweka kambi kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya
Tanzania Bara.
Klabu ya El Merreikh ya Sudan
iliyomnasa Mrisho Ngassa, nayo ilituma mwakilishi wake kwenda kuzungumza na
Umony wiki iliyopita, lakini nayo ikashindwa dhidi ya mikakati ya Azam ambayo
itawakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika
inayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).
Umony aling’ara katika michuano
ya Kombe la Chalenji iliyomalizika Jumamosi jijini Kampala, Uganda na kuibuka
Mchezaji Bora wa michuano hiyo mwaka huu baada ya kuonyesha kiwango safi na
kufunga magoli matatu yaliyoisaidia Ugandae kutwaa ubingwa.
Alirejea Uganda na kujiunga na
KCC baada ya kumaliza mkataba wake na klabu ya Becamex Binh Duong ya Vietnam.
Aliwahi pia kuzichezea klabu za SuperSport United ya Afrika Kusini, klabu ya
Chuo Kikuu cha Pretoria ya Afrika Kusini na pia akaichezea kwa mkopo wa mwaka
mmoja klabu ya Portland Timbers ya Marekani.
No comments:
Post a Comment