Wilfred Zaha |
LONDON, England
WILFRED Zaha amekuwa mchezaji wa pili kutoka Ligi Daraja la Kwanza kuitwa katika timu ya taifa ya England katika kipindi cha miaka mitano wakati mshambuliaji huyo alipojumuishwa kwenye kikosi kitakachocheza mechi ya kesho ya kirafiki dhidi ya Sweden kufuatia kujitoa kwa wachezaji watano wikiendi.
Zaha, ambaye alisherehekea kutimiza umri wa miaka 20 Jumamosi, ameisaidia Crystal Palace kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi daraja la kwanza, na anajumuika na beki wa Arsenal, Carl Jenkinson na kiungo wa Tottenham Hotspur, Tom Huddlestone baada ya Wayne Rooney, Theo Walcott, Jonjo Shelvey, Kyle Walker na Aaron Lennon kujitoa kutokana na kuwa majeruhi.
Jenkinson, ambaye ameanza katika kikosi cha kwanza cha Arsenal mara 8 katika ligi kuu ya England msimu huu, amejumuishwa baada ya kupata kibali cha FIFA kufuatia awali kuiwakilisha timu ya taifa ya vijana ya Finland kutokana na utaifa wa mama yake.
Zaha, ambaye wiki iliyopita alipigiwa simu na nahodha wa Ivory Coast, Didier Drogba, ili akaiwakilishe nchi yake hiyo aliyozaliwa kwenye fainali za Mataifa ya Afrika Januari, ameichezea timu ya taifa ya vijana ya England ya U-21 mara tano, na anakuwa mchezaji wa pili kuitwa taifa England tangu Jay Bothroyd, ambaye wakati huo alikuwa akiichezea Cardiff City, mwaka 2010.
Nyota huyo anajumuika kwenye orodha ya wachezaji wengine wenye vipaji walioshawishiwa kuzitosa nchi za asili yao ili waichezee England akiwamo straika wa Manchester United, Danny Welbeck na winga wa Liverpool mwenye umri wa miaka 17, Raheem Sterling ambaye haraka amewahishwa kuingia katika timu ya wakubwa ili akishaichezea England asiwe tena na uwezo wa kuichagua nchi ya asili yake ya Jamaica
No comments:
Post a Comment