Tuesday, November 20, 2012

WANAJESHI WALIOMUUA SWETU FUNDIKIRA WAHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA... NI SAJENTI RHODA ROBERT, KOPLO ALLY NGUMBE NA MOHAMED RASHID... MAREHEMU ALIUAWA SAA 7:30 USIKU KATIKA BARABARA YA MWINJUMA, ENEO LA KINONDONI JIJINI DAR ES SALAAM... TAZAMA NA MAPICHA TELE KUHUSIANA NA HALI ILIVYOKUWA KORTINI

Wauaji Ali na Mohamed wakitolewa kutoka ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo baada ya kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua Swetu Fundikira..

Wanajeshi watatu waliokutwa na hatia ya mauaji na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa leo.

Marehemu Swetu Fundikira ambaye aliuawa na wanajeshi wa JWTZ.

Wanajeshi waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa, Mohamed (kushoto) na Ally wakitolewa nje ya mahakama baada ya hukumu yao leo Nov.20, 2012.

Ali akiaga ndugu na jamaa zake mahakamani baada ya kuhukumiwa kunyongwa mbele ya Jaji Zainab wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo Novemba 20, 2012.

Sajenti Rhoda (kulia) akitolewa kizimbani baada ya kuhukumiwa kunyongwa kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo Novemba 20, 2012.

Panda hukooo...! Sajenti Rhoda akiongozwa na askari magereza kukwea karandinga baada ya kuhukumiwa kunyongwa kwa kumuua Swetu Fundikira leo Novemba 20, 2012.

Wanajeshi waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa, Ali (mwenye kanzu na barghashia mbele) na Mohamed (mwenye kanzu nyuma) na Sajenti Rhoda aliyevalia gauni jekundu (nyuma0 wakitolewa kizimbani baada ya kuhukumiwa kunyongwa leo Novemba 20, 2012.

Ali na Mohamed wakiongozwa kupanda karandinga baada ya kuhukumiwa kunyongwa na Jaji Zainab wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo Novemba 20, 2012.

Wanajeshi Ali (kulia) na mwenzake Mohamed wakikwea karandinga baada ya kuhukumiwa kunyongwa baada ya kukutwa na hatia ya kuua kwa kukusudia leo Novemba 20, 2012.

Baadhi ya ndugu wa marehemu Swetu Fundikira wakishangilia baada ya Jaji Zainab kuwahukumu kunyongwa hadi kufa wanajeshi watatu waliomuua ndugu yao. Hapa ni nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo (Novemba 20, 2012) baada ya kutolewa kwa hukumu ya kesi hiyo iliyovuta hisia za wengi.

Ndugu wa marehemu Swetu Fundikira wakiendelea kushangilia baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo (Nov. 20, 2012) kuamuru kunyongwa hadi kufa kwa wanajeshi watatu waliomuua ndugu yao.

Wale askari watatu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji dhidi ya Swetu Fundikira ambaye ni mtoto wa kigogo wa zamani wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa leo baada ya kukutwa na hatia kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Waliokumbwa na hukumu hiyo ya kunyongwa hadi kufa iliyotolewa na Jaji Zainabu Miruke ni Sajent Rhoda Robert, Koplo Ally Ngumbe na Mohamed Rashid. Marehemu Swetu alikuwa ni mtoto wa Chifu Abdallah Said Fundikira, mmoja wa viongozi wa juu katika serikali ya awamu ya kwanza ya Tanzania.

Watu kibao walifurika kwenye ukumbi wa mahakama kuanzia mishale ya saa 2:00 asubuhi kusikiliza kesi hiyo iliyokuwa gumzo.

Jaji Zainab aliingia mahakamani mishale ya saa 4:45 kabla ya kuanza kusoma hukumu hiyo. Akasema washitakiwa wanatuhumiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia.

Jaji akaongeza kuwa Oktoba 5, 2011, washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo na waliposomewa mashitaka yao na maelezo ya awali, walikana na kukubali tu kwamba majina na vyeo vyao jeshini ndivyo vilivyokuwa sahihi.

Mashahidi sita waliitwa na upande wa Jamhuri na ikathibitika kupitia maelezo yao kuwa kweli, washtakiwa walifanya mauaji ya kukusudia dhidi ya Swetu.

Jaji Zainab akaongeza kuwa mbali na maelezo ya ushahidi, upande wa mashitaka ulitakiwa pia kuthibitisha mambo manne ambayo ni kufa kwa Swetu, kufa kwa Swetu kwa kifo ambacho si cha kawaida, kuhusika kwa washtakiwa katika kifo hicho na pia kuieleza mahakama kama washtakiwa waliua huku wakiwa na nia ovu.

Jaji akasema kuwa upande wa Jamhuri ulipaswa kuithibitishia mahakama namna nia ovu ilivyotumika ikiwamo kueleza kama washtakiwa walitumia silaha, aina ya silaha waliyotumia, nguvu iliyotumika ili kutimiza nia ovu, tabia ya washtakiwa kabla na baada ya tukio na majeraha mangapi walimsababishia marehemu.

Akasema katika maelezo ya shahidi wa nne ambaye ni daktari aliyechunguza mwili wa marehemu, ilithibitika kuwa Swetu alikufa kutokana na majeraha yaliyotokana na kupigwa na kitu chenye ncha kali.

Hata hivyo, Jaji Zainab akasema hakukuwa na shahidi aliyethibitisha kuwa aliwaona washtakiwa wanavyomuua Swetu, bali mashahidi watatu walithibitisha kuwaona washtakiwa wakiwa na Swetu kabla ya kukutwa na umauti.

Akasema ushahidi wa mazingira unatakiwa uwe kwenye mtiririko ambao utatoa jibu moja, na ndivyo ushahidi ulivyoonesha kuwa washtakiwa walimuua Swetu kutokana na mazingira ambayo ushahidi wake ulikuwa mmoja dhidi ya washtakiwa.

Jaji akasema kuwa kwenye kesi hiyo, ushahidi wa mazingira umeowanyooshea kidole washtakiwa moja kwa moja, wanahusika na mauaji hayo na hivyo akawatia hatiani na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa

Kabla Jaji Zainab kutoa hukumu yake, wakili wa utetezi, Kaloli Mluge, aliomba mahakama iwahurumie kwa kuwapunguzia adhabu kwani umri wao ni mdogo na bado wanahitajika kwa ujenzi wa taifa na pia familia zao.

Hata hivyo, Jaji Zainab akasema kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, pasi na kuacha shaka, mahakama imewatia hatiani washtakiwa na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa.




Baada ya hukumu kutolewa, ndugu na jamaa kibao wa marehemu Swetu waliofurika mahakamani hapo walilipuka kwa shangwe na vigelele kwa kujifariji kuwa hatimaye haki imetendeka. Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa ndugu na jamaa za askari waliohukumiwa kunyongwa kwani wao walionekana wakilia kwa uchungu na kuonekana kama wasioamini juu ya kile kilichotokea.    

Washtakiwa walidaiwa kutenda kosa hilo Januari 23, 2010, mishale ya saa 7:30 usiku katika barabara ya Mwinjuma, eneo la Kinondoni jijini Dar es Salaam. Walifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Januari 27, 2010, mbele ya Hakimu Mkazi, Genivitus Dudu kwa usikilizwaji wa awali. Upelelezi ulipokamilika, kesi hiyo ikahamishiwa kwenye Mahakama Kuu.

Wakili wa upande wa uetetezi uliokuwa na mashahidi watatu, Mluge, alisema kuwa hajaridhika na hukumu ya Jaji zainab na hivyo watakata rufaa.

Washtakiwa walimuua kwa makusudi Swetu Januari 23, mwaka 2010, saa 7:30 usiku Kinondoni katika barabara ya Mwinjuma.

1 comment:

  1. I think its high time Tanzania should abardon death sentence on road rage otherwise alot of people will die just imagine 1 = 3 not fair.

    ReplyDelete