Sheikh Ponda akifunguliwa pingu kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi, Novemba 1, 2012. |
Askari wa kikosi cha farasi wakizuia waumini wa dini ya Kiislamu waliofika mahakamani kuhuhudhuria kesi ya Sheikh Ponda leo Alhamisi Novemba 1, 2012. |
Sheikh Ponda na wenzake wakiongozwa kutoka ndani ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Novemba 1, 2012.
Sheikh Ponda akiwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Novemba 1, 2012. |
Baadhi ya Waislamu walioshtakiwa pamoja na Sheikh Ponda wakifunguliwa pingu kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi Novemba 1, 2012. |
Mshtakiwa mmojawapo miongoni mwa Waislamu 49 walioshtakiwa pamoja na Sheikh Ponda akiwa amebebwa na mwenzake baada ya kudondoka mahakamani na kupoteza fahamu leo Alhamisi Novemba 1, 2012. |
Polisi wa kikosi cha mbwa pia walimwagwa kwenye Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam leo wakati wa kutajwa kwa keshi ya Sheikh Ponda na Waislamu wengine 49. |
Ukaguzi wa kila mtu kwa vifaa maalum ukiendelea kwenye geti la kuingilia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi, Novemba 1, 2012. |
Polisi wa Mbwa wakisubiri amri ndani ya gari lao nje ya mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, leo Alhamisi Novemba 1, 2012 |
Polisi
wa Mbwa akifanya doria kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Novemba 1, 2012 wakati wa kutajwa kwa kesi ya Sheikh Ponda. |
Utitiri wa askari polisi wa kawaida, FFU,
Magereza na wengine wa upelelezi waliovalia kiraia walimwagwa kwenye Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo wakati wa kutajwa kwa kesi
inayomkabili Sheikh Ponda Issa Ponda na Waislamu wengine 49.
Katika eneo la mahakama kulikuwa pia na
utitiri wa mbwa, farasi na magari yaliyosheheni askari zaidi kwa nia ya
kuimarisha usalama.
Ponda na wenzake wanakabiliwa na mashitaka
matano ambayo ni pamoja na kula njama, kuingia, kujimilikisha ardhi kwa jinai na
wizi wa mali ya Sh. milioni 59.6. Sheikh
Ponda pia anakabiliwa na shitaka la uchochezi.
Watu waliokuwa wakipita kwenye lango la
kuingilia mahakamani hapo walikuwa wakikaguliwa kila mmoja kwa mitambo maalum.
Kuanzia mishale ya saa 2:00 asubuhi, askari zaidi wenye sare za polisi na
magereza waliomgezeka eneo la mahakama huku wakiwa na silaha na zana mbalimbali
za kukabiliana na tishio lolote la uvunjifu wa amani.
Wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo, Hakimu
Mkazi, Victoria Nonga, aliwasomea washtakiwa 49 masharti ya dhamana isipokuwa
Sheikh Ponda ambaye ni mshtakiwa namba moja kwa maelezo kwamba Mkurugenzi wa
Mashtaka Tanzania (DPP) ameendelea kuweka pingamizi kuzuia dhamana yake.
Washtakiwa wengine walitakiwa kuwa na
mdhamini mmoja kila mmoja atakayesaini hati ya dhamana ya Sh. milioni moja na
kila mmoja angeachiwa kama angetimiza masharti hayo. Hata hivyo, wote
walirejeshwa rumande pamoja na Sheikh Ponda baada ya kile kilichoelezwa kuwa ni
kutotimiza masharti waliyopewa. Kesi hiyo itatajwa tena Alhamisi ya Novemba 15.
Awali, wakili mwandamizi wa serikali,
Tumaini Kweka, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba
Mahakama kupanga tarehe ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Sheikh Ponda na wenzake 49 walifikishwa
mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Oktoba 18 mwaka huu na kusomewa mashtaka
kabla DPP kuwasilisha hati ya kiapo cha kupinga dhamana ya Sheikh Ponda kwa
maslahi ya taifa.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni
Seleman Wajumbe, Salum Juma, Salum Mkwasu, Ramha Hamza, Halima Abas, Maua
Mdumila, Fatihiya Habibu, Hussein Ally
na Kurthum Mohamed, Zaldah Yusuph, Juma
Mpanga, Farida Lukoko, Adamu Makilika na Athumani Salim.
Wengine ni Alawi Alawi, Ramadhani
Mlali, Omary Ismaili, Salma
Abduratifu, Khalidi Abdallah, Said Rashid, Shaban Ramadhani, Hamis Mohamed,
Rashid Ramadhani, Yusuph Penza, Feswali
Bakari, Issa Wahabu, Ally Mohamed, Abdallah Senza, Juma Hassani, Mwanaomary Makuka na Mohamed Ramadhani.
Wengine ni Smalehes Mdulidi, Jumanne Mussa,
Salum Mohamed, Hamis Halidi, Dite Bilali, Omary Bakari, Maulid Namdeka, Farahan Jamal, Amiri Said, Juma Yassin, Rashid Ndimbu, Hamza Ramadhani, Ayubu Juma, Athuman Rashid,
Rukia Yusuph, Abubakar Juma na Ally Salehe.
Awali, upande wa mashtaka ulidai kuwa katika
shtaka la kwanza, Oktoba 12, 2012,
katika eneo la huko Temeke jijini Dar es Salaam, Sheikh Ponda na wenzake
walikula njama ya kutenda makosa.
Shitaka la pili linadai kuwa siku ya tukio
la kwanza, eneo la Chang’ombe Markas, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam,
washtakiwa hao kwa jinai walivamia kwa nia ya kutaka kujimilikisha kiwanja
ambacho ambacho ni mali ya kampuni ya Agritanza.
Katika shitaka la tatu, imedaiwa kuwa kati
ya Oktoba 12 na 16, 2012, katika eneo la Chang’ombe Markas, pasipo uhalali,
washtakiwa walijimilikisha ardhi hiyo.
Katika shtaka la nne, imedaiwa kuwa kati ya
Oktoba 12 na 16, mwaka huu, karika eneo hilo, washtakiwa waliiba vifaa
mbalimbali vya ujenzi yakiwamo matofali 1,500, tani 36 za kokoto na nondo
vyenye thamani ya Sh. 59,650,000.
Shtaka la tano lililodaiwa ni Jamhuri ni
kuwa, kati ya Oktoba 12 na 16 mwaka huu, eneo la Chang’ombe Markas, Sheikh
Ponda akiwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania, aliwashawishi
wafuasi wake kutenda makosa ya jinai. Washtakiwa wote wamekana mashtaka.
Eneo la Markas lililomponza Sheikh Ponda na
Waislamu wengine 49 waliokuwa wameweka kambi eneo hilo lilikuwa likimilikiwa na
Waislamu kupitia Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa ajili ya
shughuli mbalimbali zikiwamo za kujengea chuo kikuu, lakini inadaiwa kuwa
baadaye likauzwa.
No comments:
Post a Comment