Wednesday, November 28, 2012

PENATI YA SELEMANI NDIKUMANA YAIMALIZA KILI STARS KOMBE LA CHALENJI JIJINI KAMPALA LEO… NI STRAIKA WA ZAMANI WA KLABU YA SIMBA… JOHN BOCO ADEBAYOR AGONGESHA MWAMBA KUWAKOSAKOSA MARA KIBAO... MRISHO NGASSA AWAKIMBIZA WEE LAKINI MIPIRA YAKATAA KUTINGA WAVUNI!


Mshambuliaji wa timu ya Kilimanjaro Stars, Simon Msuva akimiliki mpira wakati wa mechi yao ya Kundi B la michuano ya Cecafa Challenge dhidi ya Burundi kwenye Uwanja wa Namboole mjini Kampala leo. Kili Stars ililala 1-0.

PENALTI iliyopigwa kifundi na straika wa zamani wa Simba, Selemani Ndikumana ilitosha kuipa Burundi ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ katika mechi yao ya Kundi B la Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Namboole mjini Kampala leo.

Stars licha ya kulala leo, imebaki katika nafasi ya pili kutokana na pointi 3, ilizozipata kwa kuifunga Sudan 2-0 katika mechi ya ufunguzi wa kundi hilo Jumapili.

Sudan pia imeendelea kubaki katika nafasi ya tatu licha ya kushinda 1-0 dhidi ya Somalia katika mechi iliyopiga mapema leo kwenye uwanja huo uliojaa matope na kuchimbika kama wa mchezo wa "rugby".

Kili Stars itacheza mechi yake ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Somalia Jumamosi, itakayotanguliwa na mechi nyingine ya kundi hilo baina ya Burundi na Sudan.

Timu mbili kutoka kila kundi kati ya matatu yaliyopo zinafuzu moja kwa moja hatua ya robo fainali na timu mbili zitakazoshika nafasi ya tatu zikiwa na matokeo mazuri zaidi zitakamilisha timu nane za robo fainali.

Ndikumana ambaye aliwahi kuichezea klabu ya Simba ya Dar es Salaam alifunga penalti hiyo ya dakika ya 52 iliyotolewa na refa Ronnie Kalema wa Uganda baada ya beki wa kati wa Kili Stars, Shomary Kapombe kumuangusha nyota huyo aliyekuwa akienda kufunga.

Kapombe alionekana akijikwaa na kuanguka kabla ya kumgusa kwa goti straika huyo, tukio ambalo lilimuumiza vibaya beki huyo wa klabu ya Simba ambaye alitolewa kwa machela na hakurudi tena uwanjani.

Nafasi ya Kapombe ilichukuliwa na beki wa kulia Issa Rashid 'Baba Ubaya'. Erasto Nyoni aliyekuwa akicheza kulia, alihamia katika nafasi ya ulinzi wa kati kwa ajili ya kushirikiana na Kelvin Yondani.

Ushindi umeifanya Burundi itinge hatua ya 8-Bora kutokana na kufikisha pointi 6. Katika mechi yao ya walishinda 5-1 dhidi ya Somalia.

Winga wa Kili Stars, Mrisho Ngassa aliwatesa mabeki wa Burundi na kipa wao kutokana na kuwazidi kila wakati na kupiga mashuti ambayo yalimnyima usingizi kipa huyo ambaye aliokoa hata nyingi kishujaa.

Amri Kiemba, aliyeingia mapema katika dakika ya 36 kuchukua nafasi ya mshambuliaji Simon Msuva, alileta uhai mkubwa katika kikosi cha Poulsen akipiga mashuti mawili ya hatari kabla ya mapumziko.

Stars ilimpoteza kiungo Mwinyi Kazimoto ambaye aliumia baada ya kukanyagwa vibaya na mchezaji wa Burundi na nafasi yake ilichukuliwa na Shaaban Nditi.

Straika wa Kili Stars, John Bocco 'Adebayor' alikuwa hatari langoni mwa Burundi akifanya majaribio kadhaa ambayo yalidakwa kishujaa na kipa wa wapinzani ikiwamo 'tik-taka' ambayo Watanzania walidhani inakwenda wavuni.

Nafasi kubwa zaidi kwa Bocco ilikuja katika dakika ya 89 wakati mpira wa kichwa alioupiga ulipogonga 'mtambaa panya' na kuokolewa juu ya mstari na beki wa Burundi wakati ukielekea wavuni huku kipa akiwa tayari ameshakubali matokeo.

Kocha Poulsen aliwapongeza wachezaji wake kwa kiwango walichoonyesha huku akisema kama wataendelea kupambana kwa staili ile watafika mbali.

"Kwanza niwapongeze wapinzani wetu kwa ushindi. Halafu niwapongeze pia wachezaji wangu kwa kukuendelea kuliandama lango la Burundi bila ya kuchoka. Walikuwa na bahati wakati sisi tulikosa bahati. Tumepiga mashuti zaidi ya 20 lakini bahati haikuwa kwetu," alisema Poulsen.

Kocha msaidizi wa Burundi, Amars Niyongabo, alikiri kwamba walilazimika 'kupaki basi' kuelekea mwishoni mwa mechi kwa kuihofia Stars ambayo iliwafunga wakati walipokutana kwa mara ya mwisho.

Kikosi cha Stars kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe/ Issa Rashid (dk. 52), Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Salum Aboubakar 'Sure Boy', John Bocco 'Adebayor', Mwinyi Kazimoto/ Shaban Nditi (dk.69) na Simon Msuva/ Amri Kiemba (dk.36).


No comments:

Post a Comment