Emmanuel Adebayor |
STRAIKA Emmanuel Adebayor wa klabu ya Tottenham ya England ametishia kujiengua katika soka la kimataifa ikiwa Shirikisho la Soka la Togo (TFF) litaendelea na tabia ya kutowalipa posho zao wachezaji wa timu ya taifa hilo.
Adebayor alisema kuwa hadi sasa, wachezaji wa timu ya taifa ya Togo waliocheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Morocco mwezi huu bado hawajalipwa posho zao na hivyo ameonya kuwa yeye hataichezea tena timu hiyo ikiwa tabia hiyo haitakomeshwa.
"Kama tabia hii isipokoma, mimi nitastaafu kucheza soka la kimataifa na wachezaji wengi wengi wataacha kuichezea timu ya taifa ya nchi yetu," Adebayo amekaririwa na redio ya Togo ya Frequence1.
"Katika chama chetu cha soka, kila mmoja anafikiria kutunisha mifuko yake. Baadhi ya wachezaji hawajapata fedha zao za posho, baadhi wamelipwa nusu.
"Wachezaji wamenijia na kuniuliza kuhusu fedha zao. Ni aibu. Niliwauliza Shirikisho la Soka la Morocco ni kiasi gani wamelipa kwa Chama cha Soka cha Togo (FA). Wakaniambia kwamba walilipa euro 35,000 (Sh. milioni 70) kwa rais wa FA, Ameyi.
"Rais anazo fedha kwa sababu FA ya Morocco hawawezi kunidanganya. Kama hali hii itaendelea, basi hakuna yeyote atakayekuwa tayari kucheza kwa nia ya kutunisha mifuko ya wengine," ameongeza Adebayor.
No comments:
Post a Comment