Mourinho kulia (kulia) |
Rais wa PSG, Nasser Al Khelaifi. |
Kuna taarifa kuwa klabu ya PSG ya Ufaransa inamfukuzia kocha Jose Mourinho kwa udi na uvumba na kwamba hadi sasa, tayari imeshamtega kwa kumuahidi 'ofa' ya hundi iliyo wazi ili ajaze mwenyewe kiasi chochote cha 'mihela' anayoitaka ili aachane na klabu yake ya sasa ya Real Madrid na kwenda kuipa mataji klabu hiyo ya Ufaransa.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari hivi karibuni, Mourinho alisema kwamba atakaa chini na uongozi wa Real Madrid mwishoni mwa msimu (Juni, 2013) na kuangalia kama pande zote zinaridhia kuendelea kufanya kazi pamoja ama la. Matukio ya hivi karibuni yameibua uvumi kuhusiana na hatma ya kocha huyo Mreno.
Nasser Al Khelaifi ndiye Rais wa PSG. Ni mtu wa karibu wa sheikh wa Qatar aliyeinunua klabu hiyo na amepewa mamlaka ya kumsajili kocha au mchezaji yeyote wamtakaye.
Mbali na ofa ya ajabu ya kumpa hundi nyeupe ili ajaze mwenywe kiasi cha fedha anachotaka, wamiliki hao wa Qatar wanajua kuwa Mourinho siku zote huwa na mahitaji ya ziada kila mara anapojiunga na klabu mpya na wao wako tayari kumsikiliza.
Wamempa ofa ya kuwa na mamlaka ya kusimamia shughuli za soka na pia mambo ya fedha ili asajili mchezaji yeyote amtakaye na pia kuachana na yeyote atakayemuona kuwa hamfai.
Hata hivyo, katika mahojiano yake na gazeti la MARCA linalotolewa Madrid nchini Hispania, Nasser Al Khelaifi alimwagia sifa Mourinho na kusema wazi kwamba, wakielekea nusu ya msimu huku Ancelotti akiongoza timu yao, hafikirii suala hilo: "Mourinho ni kocha mwenye akili sana na anafanya kazi nzuri Real Madrid. Tunaridhishwa na Ancelotti na hatufikirii kuhusu kubadili kocha".
No comments:
Post a Comment