Saturday, November 3, 2012

MWANDISHI WA KAMPUNI YA BUSINESS TIMES APIGWA RISASI NA MAJAMBAZI NA KUJERUHIWA VIBAYA... ALIVAMIWA WAKATI AKITOKA OFISINI KWAO MTAA WA LUGODA KUELEKEA NYUMBANI KWAKE MBAGALA... WAVAMIAJI WAPORA FUNGUO YA GARI ALILOKUWA NALO... RISASI YAPENYA MDOMONI NA KUTOKEA UPANDE MWINGINE... AKIMBIZIWA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI AKIWA HOI...!

Akiwa hospitalini baada ya kujeruhiwa kwa risasi.
Akiwa hospitalini.
Mwandishi wa habari aitwaye Mnaku Mbani Lukanga wa kampuni ya Business Times ya jijini Dar es Salaam amevamiwa usiku huu na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi na kupigwa risasi iliyomjeruhi vibaya na kukimbiziwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili akiwa hoi, imefahamika.

Taarifa ambazo Straika imezipata kupitia vyanzo mbalimbali, zinaeleza kuwa mwandishi huyo ambaye pia ana cheo cha uhariri katika moja ya magazeti ya kampuni ya Business Times yenye ofisi zake katika Mtaa wa Lugoda, amepigwa risasi mdomoni na kutokea upande mwingine wa kinywa, hivyo kumjeruhi vibaya na kumng'oa meno yasiyopungua matatu.

Imeelezwa zaidi kuwa tukio hilo limetokea wakati mwandishi huyo akiwa njiani kutoka kazini (Mtaa wa Lugoda) kuelekea nyumbani kwake Mbagala; ambapo akiwa njiani, majambazi yalimvamia na kumpora funguo ya gari kabla mporaji mwingine hajampiga risasi iliyomjeruhi vibaya.

Hakukuwa na taarifa zaidi za kipolisi kuelezea tukio hilo kiundani.

No comments:

Post a Comment