Lionel Messi |
Cristiano Ronaldo |
Andres Iniesta |
Nyota
wa Barcelona, Lionel Messi na Andres Iniesta na wa Real Madrid, Cristiano
Ronaldo walitangazwa kuwamo katika orodha ya wachezaji watatu watakaochuana
kuwania Tuzo ya Mwanasoka Bora wa FIFA (FIFA Ballon d'Or) katika mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika leo nchini Brazil.
Muargentina
Messi ameshinda tuzo hiyo, zamani ikijulikana kama Tuzo ya Mwanasoka Bora wa
Mwaka wa Dunia, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na sasa anapewa
nafasi kubwa ya kushinda tena baada ya kuendelea na kasi yake ya kufunga magoli
‘atakavyo’.
Messi
na Ronaldo ambaye pia hufunga magoli kama mvua, mara kwa mara wamekuwa
wakibishaniwa kuwa ni nani mkali zaidi ya mwingine kati yao na mwaka huu hauna
tofauti kwani wanaonekana kuchuana vikali zaidi katika kila wiki.
Kocha
wa Ronaldo katika klabu ya Real Madrid, Jose Mourinho, alisema hivi karibuni
kwamba itakuwa ni kosa la jinai ikiwa mchezaji wake hatashinda Tuzo ya Ballon
d'Or kwa mara ya pili, ikiwa ni baada ya maoni kutoka kwa kocha wa Barcelona, Tito Vilanova aliyemuelezea Messi kama "mchezaji
mkali kuliko wote duniani, kwa tofauti kubwa kulinganisha na wengine ".
"Kama
Messi ndiye bora zaidi duniani, Ronaldo ni bora zaidi ulimwenguni. Itakuwa ni
kosa la jinai ikiwa Ronaldo hatashinda Tuzo ya Ballon d'Or," Mourinho alisema
Oktoba, muda mfupi baada ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ureno kuwa
mchezaji wa kwanza kuwahi kufunga magoli katika mechi sita mfululizo za 'Clasico',
ambazo huwakutanisha mahasimu wa jadi Barcelona na Real Madrid.
Messi
alifunga magoli 50 katika La Liga, Ligi Kuu ya Hispania msimu uliopita, manne
zaidi ya Ronaldo, na ameshafunga magoli 82 katika mwaka wa kalenda hadi sasa, yakibaki
magoli matatu kabla ya kuifikia rekodi ya magoli 85 iliyowekwa na Gerd Mueller mwaka
1972.
Hata
hivyo, Ronaldo ambaye ni mshindi wa tuzo hiyo mwaka 2008 alikuwa mhimili wa Real
Madrid katika safari yake ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya Hispania msimu uliopita
na pia kuisaidia Ureno kufika nusu
fainali ya michuano ya Euro.
Iniesta
ndiye mchezaji pekee kati yao aliyetwaa taji la Kombe la Dunia na mataji mawili
ya Euro akiwa na timu yake ya taifa ya Hispania.
Kama
Messi atashinda tuzo hiyo mjini Zurich Januari 7, atakuwa mwanasoka wa kwanza kushinda
tuzo hiyo mara nne mfululizo.
Wanaowania
Tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka wa Dunia ni kocha wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente
del Bosque, kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola na Mourinho.
Alex
Morgan na Abby Wambach wa timu ya taifa ya Marekani na Mbrazil Martha wametajwa katika orodha ya
nyota watatu watakaowania Tuzo ya FIFA ya Mwanasoka Bora Mwanamke wa Mwaka wa
Dunia.
Uteuzi
huo umetokana na kura ambazo zimepigwa na manahodha na makocha wa timu za taifa
za soka za wanaume na wanawake, pamoja na vyombo vya habari teule.
No comments:
Post a Comment