Tuesday, October 9, 2012

Wakali wa kurap, DJ Bora wapatikana Mbeya

Mfalme wa ma-Mc mkoani Mbeya, Godfrey Ammon akionyesha tuzo yake aliyokabidhiwa wa Meneja wa TCC Tawi la Mbeya, Jacob Ndaga (kulia) wakati wa Tamasha la Str8Muzik Freestyle 2012 lililofanyika Mbeya Jumamosi.

Na Mwandishi Wetu
MASHINDANO ya vipaji vya kurap kwa "michano huru" na ya kumsaka DJ bora yalimalizika mkoani Mbeya Jumamosi kwa Yusuph Jeremiah kutwaa taji la DJ Bora, huku Godfrey Ammon akishinda tuzo ya rapa (MC) bora.

Mchakato wa kuwasaka wakali hao katika Tamasha la Str8Muzik Freestyle 2012 ulianza Septemba 27 mjini Mbeya na kumalizika Jumamosi iliyopita katika mpambano mkali huku kila mshiriki akidhamiria kunyakua zawadi ya juu kabisa.

Baada ya kutangazwa mshindi, Jeremiah alikabidhiwa mashine mpya ya u-DJ yenye thamani ya Sh. milioni 7 na tuzo wakati Ammon alipata nafasi ya kurekodi  nyimbo tatu kwa watayarishaji wa muziki watatu wa chaguo lake na kazi zake kutangazwa katika moja ya redio kubwa nchini kwa miezi sita mfululizo.

Mshindi wa pili kwa upande wa ma-DJ alikuwa Burhani Said aliyepata Sh. 100,000 na mfuko wa safari wenye zawadi mbalimbali na mshindi wa pili upande wa ma-Mc naye alipokea kiasi kama hicho cha fedha na zawadi mbalimbali.

Ma-DJ watano walioshiriki katika fainali hizo ni Burhani Said, Newton Hezron, Yusuph Jeremiah, Michael Fadhili na Mozati Mbena.

Burhani Saidi, Michael Fadhili na Yusuph Jeremiah waliingia nusu fainali huku Said na Jeremiah wakitinga fainali na baadaye Jeremiah alitangazwa kuwa ndiye DJ bora wa Mkoa wa Mbeya.

Marapa wa "michano huru" wanane walioshiriki katika fainali hiyo ni  Mtafya Mwampamba, Yusuph Sajo, Mandenda Mikidadi, Selemani Victor, Baraka Nelson, Gordon David, Godfrey Ammon na Julius Nyandindi.

Selemani Victor, Godfrey Ammon, Mtafya Mwampamba na Mandenda Mikidadi waliingia nusu fainali. Mpambano huo ulikuwa mkali sana hivi kuwalazimu majaji kuwaomba baadhi ya washiriki wachuane tena kabla hayajatangazwa majina mawili ya Victor na Ammon ambao walitinga fainali na baadaye Ammon kutangazwa mshindi.

"Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa sababu amenisaidia kimeonekana. Mwaka jana nilishiriki lakini sikufanikiwa kushinda hivyo nikaamua kufanya maandalizi makubwa zaidi na kweli nimeshinda,” alisema Jeremiah huku akiwa na furaha.

“Nawashukuru waandaaji kwa kutuwezesha kwani sasa wengine wetu tutaweza kufikia baadhi ya malengo yetu,” alisema Ammon huku akiwa ameshika tuzo yake.

Tamasha la Str8MuzikFreestyle lilifanyika Mjini Mwanza wiki mbili zilizopita na baadaye mwezi huu litafanyika Jijini Dar es Salaam ambapo ma-DJ and Ma MC bora watajulikana.

No comments:

Post a Comment