Wednesday, October 17, 2012

SIMBA YAKABWA KOO NA WABABE WA YANGA

Benjamin Effe wa Kagera Sugar akiwania mpira dhidi ya Mrisho Ngassa wa Simba wakati mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. Timu hizo zilitoka sare ya 2-2. Picha: Bongostaz.blogspot.com
MABINGWA Simba walipoteza uongozi magoli ndani ya dakika 3 na kuruhusu sare ya 2-2 dhidi ya Kagera Sugar katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

Licha ya sare hiyo, Simba inaendelea kung'aa kileleni mwa msimamo kutokana na kuwa na pointi 18, moja zaidi ya Azam, ambao wamebaki katika nafasi yao ya pili baada ya nao kulazimishwa sare ya 0-0 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Simba wamecheza mechi 8 wakati Azam imecheza 7.


JKT Ruvu imeifunga 2-0 Polisi Moro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, JKT Oljoro imelazimishwa sare ya 0-0 dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, wakati Mgambo JKT imeshinda 2-0 dhidi ya Toto African ya Mwanza kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga. Ulikuwa ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Mgambo ambao walikaribishwa kwenye ligi kuu waliyopanda msimu huu kwa vipigo vipigo vinne mfululizo.


Simba ambayo ilifurahia kurejea kikosini kwa nyota wake watatu, Emmanuel Okwi aliyekuwa akiitumikia timu yake ya taifa ya Uganda, winga Mrisho Ngassa aliyekuwa majeruhi na beki Amir Maftah aliyekuwa akitumikia adhabu ya kadi, walianza mechi kwa kishindo na kupata goli la mapema katika dakika ya 8 kupitia kwa straika Mzambia Felix Sunzu aliyemalizia pasi ya Ngassa.

Dakika tano baada ya mapumziko, Simba walikuwa mbele kwa magoli 2-0 baada ya Ngassa kutupia katika dakika ya 50, goli ambalo hata hivyo lilipingwa bila ya mafanikio na wachezaji Kagera Sugar ambao walidai mpira haukuvuka mstari wa lango.

Kuingia Themi Felix katika dakika 58 kuchukua nafasi ya Mnigeria Enyinna Darlington kuliiamsha Kagera Sugar na alihitaji dakika 8 tu uwanjani kuwafungia Kagera Sugar goli la kwanza kwa kichwa kufuatia makosa ya kipa Juma Kaseja aliyetoka kuufuata mpira wa kona bila ya kuwa na uhakika wa kuupata.


Themi aliyeifunga Yanga goli pekee lililowazamisha mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati wiki iliyopita mkoani Kagera, alithibitisha umuhimu wake baada ya kuubeba mpira kutoka wavuni kwa Kaseja na kuuwahisha katikati ili uanzwe haraka na ulipoanzwa Simba waliupoteza katika dakika hiyo hiyo na haraka wageni wakafika langoni mwa wenyeji.


Paul Ngwai aliyekuwa akimnyima "usingizi" beki wa Simba Nasoro Said Masoud 'Chollo' kutokana na uwezo wake mkubwa wa kukaa na mpira na kupiga chenga, aliingia kwa kasi ndani ya boksi na wakati Juma Nyosso akijaribu kumzuia akajikuta akichelewa na kuishia kumuangusha na sababisha penalti.


Beki aliyetemwa na Simba, Salum Kanoni, alimfunga nahodha wake wa zamani, Kaseja, ambaye ni maarufu kwa "kufuta" penalti, kwa shuti kali la katika ya lango.

Ilikuwa ni sare ya pili mfululizo kwa Simba ambao walianza ligi vizuri kwa kushinda mechi nne mfululizo kabla ya kushikiliwa katika sare ya kwanza dhidi ya Yanga. Kabla ya jana, walitoka sare ya 0-0 dhidi ya Coastal Union mkoani Tanga Jumamosi.


Kocha wa Kagera Sugar, Abdallah 'King' Kibadeni, nyota wa zamani wa Simba, ambaye alitumia wiki nzima akizituhumu klabu kubwa za Tanzania kwa kutoa rushwa ili kushinda mechi zao, alisema baada ya mechi hiyo kuwa amewamudu wapinzani wao kwa sababu anawafahamu vyema na pia anafahamu jinsi kocha wao Mserbia Milovan Cirkovic anavyoifundisha timu yake.


Mjini Morogoro JKT Ruvu wamepata ushindi wa 2-0 dhidi ya Polisi Dodoma kupitia magoli ya Jimmy Shoji aliyefunga katika dakika ya 26 kufuatia piga nikupige langoni mwa wenyeji na Jacob Mambia aliyewachomoka mabeki wa Polisi na kufunga katika dakika ya 43.

Ligi hiyo itaendelea Jumamosi ambapo Yanga walio katika nafasi ya tatu kwa pointi 11 watakapocheza mechi yao ya mkononi dhidi ya Ruvu Shooting jijini Dar es Salaam, huku Coastal Union, iliyo katika nafasi ya nne kwa pointi 10 itakapocheza mechi yake ya mzunguko wa nane dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani.


Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa;
Simba: Juma Kaseja, Nasoro Said 'Cholo'/ Uhuru Selemani (dk.74), Amir Maftah, Pascal Ochieng, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Haruna Moshi 'Boban'/ Jonas Mkude (dk.83), Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa.


Kagera Sugar: Andrew Ntella, Salum Kanoni, Martin Muganyizi, Amandus Nesta, Benjamin Effe, Malegesi Mwangwa, Daud Jumanne/ Kamana Salum (dk.78), George Kavila, Shija Mkina, Enyinna Darlington/ Themi Felix (dk.58) na Wilfred Emmeh/ Paul Ngwai (dk.39).


No comments:

Post a Comment