Wednesday, October 17, 2012

SHEIKH PONDA AICHANGANYA POLISI... WALAZIMIKA KUTEMBEZA MABOMU YA MACHOZI KUZUIA WATU KIBAO WALIOJITOKEZA LEO KUPINGA HATUA YAO YA KUMKAMATA NA KUMSWEKA MBARONI... MABOMU YAMWAGWA KUANZIA MAENEO YA KITUO CHA POLISI CHA KATI (POLICE CENTRAL) KUELEKEA MITAA YA MNAZI MMOJA... ABIRIA WALIOKUWA KWENYE MADALADALA NAO WAKUMBANA NA MABOMU

Yakbiiiirrrrr....! Sheikh Ponda akihamasisha jambo kwa kuinua mkono wakati akizungumza na waumini wa Kiislamu jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Si katika tukio la leo

Difenda zilizojaa askari wa FFU zikiwa tayari kwa kazi. Si katika tukio la leo


Sheikh Ponda akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari
Jeshi la Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam limelazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya watu kibao waliojitokeza leo katika maeneo ya Kituo cha Polisi cha Kati (Police Central) kupinga kukamatwa kwa Katibu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu ambaye anashikiliwa na jeshi hilo kuhusiana na kauli aliyotoa jana wakati akilaani kitendo cha hivi karibuni cha kukojolewa kwa kitabu kitukufu cha Qur-an kilichoibua vurugu kubwa katika maeneo ya Mbagala.

Mabomu hayo ya machozi yalipigwa katika maeneo ya kuanzia Police Central ambako watu hao walikuwa wakielekea kutaka kuachiwa mara moja kwa Sheikh Ponda, kuelekea Mnazi Mmoja kupitia katika mitaa mbalimbali ya maeneo ya Posta, ukiwamo wa Kitumbini.

Katika maeneo yaliyokumbwa na kadhia hiyo, maduka yalifungwa na watu wengi wameonekana wakiwa na vitambaa na maji waliyokuwa wakiyatumia kufutia machozi.

Hata baada ya umati uliojitokeza kumpigania Sheikh Ponda kutawanyika kufuatia hatua ya polisi kutembeza mabomu ya machozi, bado askari wengi wameonekana wakirandaranda huku na kule katika kile kilichoonekana kuwa ni kuhofia kuwa waumini hao watarudi tena.

Magari ya Polisi yameonekana yakipita kwa kupishana mara kwa mara katika maeneo hayo na abiria tele waliokuwamo kwenye daladala mbalimbali wakitokea 'maofisini' Posta kurejea majumbani kwao walijikuta katika wakati mgumu baada ya kukumbana na adha ya moshi wa mabomu ya machozi, ambayo kwa kawaida huwa hayachagui mtu.

Sheikh Ponda alikamatwa kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni kauli aliyoitoa wakati akizungumza na waandishi wa habari kulaani kitendo cha kijana mmoja kukojolea Qur-an tukufu na kusababisha vurugu katika maeneo ya Mbagala ambazo baadaye zilipelekea makanisa kadhaa katika maeneo hayo kushambuliwa.

Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesikika leo akiwataka wananchi kuwa watulivu na kwamba wamefanikiwa kudhibiti watu waliojitokeza kupinga kushikiliwa kwa Sheikh Ponda.

No comments:

Post a Comment