Tuesday, October 2, 2012

MTAZAME 'JINI' LIONEL MESSI ALIVYOPIGA KURA KUCHAGUA KIKOSI CHA WACHEZAJI BORA 11 WA DUNIA MWAKA 2012...!

Messi akipiga kura yake kuteua kikosi cha wachezaji bora 11 wa Dunia 2012.
Alex Song akipiga kura yake.
Xavi naye akipiga kura
'Kaka mkuu' Puyol akipiga kura yake
BARCELONA, Hispania
Lionel Messi amepiga  rasmi kura yake ya kuchagua kikosi cha Wachezaji Bora 11 wa Kulipwa wa Dunia Mwaka 2012 (FIFA/FIFPro 2012 World XI) na kuwataka wanasoka wengine nyota duniani kufanya hivyo pia.

Messi ambaye anashikilia tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia, aliwahimiza wanasoka wengine wote wa kulipwa duniani kutekeleza zoezi hilo la kuchagua kikosi hicho cha nyota 11 wa Dunia 2012.

“Nimeshachagua kikosi changu cha FIFA/FIFPro World XI. Sasa ni zamu yenu,” amesema Messi, akielekeza ushauri wake kwa wanasoka wote wa kulipwa duniani.

Tukio hilo limekuwa ni utamaduni wa kila mwaka wa FIFPro. Kila mwaka, wawakilishi wa vyama vya wanasoka wa kulipwa duniani humtembelea mshindi wa tuzo ya Mwansoka Bora wa Mwaka wa Dunia (FIFA Ballon d’Or) na kumpa nafasi ya kwanza ya kupiga kura ya kuteua kikosi cha nyota 11 wa Dunia (FIFA/FIFPro World XI). Kwa hiyo, katika mwaka wa tatu mfululizo, FIFPro wamefika Barcelona kumtembelea Leo Messi.

Mwaka huu, FIFPro inasambaza duniani kote kadi za kupigia kura 45,000. Wakisaidiwa na wanachama wa vyama vya wanasoka wa kulipwa, FIFPro watakusanya kura zitakazopigwa kutoka Asia, Amerika, Ulaya na Afrika, ambapo kila mchezaji huteua kikosi chake cha kipa, mabeki wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu.

Wachezaji wanaopigiwa kura nyingi zaidi hualikwa na kutunukiwa zawadi wakati wa hafla ya ugawaji tuzo ya Mwanasoka Bora wa mwaka wa Dunia (FIFA Ballon d’Or) zinazofanyika mjini Zurich (Uswisi), na ambazo safari hii zitafanyika Januari 7, 2013.

Messi aliiambia FIFPro: ‘Ni tuzo nzuri kwa sababu ya kuangalia maana yake, watu hupiga kura, ambao ni wanasoka wenzako wa kulipwa. Watu ambao nao hutaka kushinda ndio watu wanaochagua kikosi, hii ndiyo sababu ya kuwa tuzo hii imekuwa maalum sana."

Baada ya Messi kuteua kikosi chake, walifuatia wachezaji wengine 17 wa Barca, baadhi wakiwa ni Carles Puyol, Alex Song, Xavi, David Villa na Sergio Busquet.

"Ni heshima kubwa kuchaguliwa na wachezaji wenzako kuwa ni miongoni mwa nyota 11 wa kikosi cha Dunia (FIFA/FIFPro World XI), ni kikosi cha timu bora kabisa duniani," amesema David Villa wakati naye akipiga kura yake.

Villa alikuwamo katika miaka miwili iliyopita kwenye kikosi hicho cha nyota 11 bora wa dunia.

Tangu FIFPro ianze mwaka 2005 kuteua nyota bora 11 wa dunia katika kila mwaka, FC Barcelona imekuwa ikitoa wachezaji wengi zaidi kulinganisha na klabu nyingine zote duniani.

Mwaka jana, Dani Alves, Gerard Piqué, Andrés Iniesta, Xavi na Lionel Messi walikuwamo katika kikosi hicho. Katika misimu iliyopita, nyota kadhaa wa Barca pia walikuwamo, baadhi wakiwa ni Ronaldinho, Samuel Eto’o, David Villa na Carles Puyol.

No comments:

Post a Comment