Tuesday, October 23, 2012

MASWALI MAGUMU KUHUSU MAKATO 17 YA KINYONYAJI MECHI ZA LIGI KUU BARA

Mwinyi Kazimoto wa Simba (chini) akivuja jasho na wachezaji wengine wa JKT Oljoro kwa ajili ya kuinufaisha serikali katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

MAKATO ya ajabu ajabu, yasiyo na msingi na mengine mengi yanayofanana, ambayo yanabadilishwa-badilishwa majina tu licha ya kubeba maana moja, yameendelea kuzikamua hadi tone la mwisho klabu za ligi kuu katika kampeni "nzito" ya kuhakikisha haziendelei.

Katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom baina ya Simba na Kagera Sugar iliyochezwa Oktoba 17 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2, Sh. milioni 58.5 zilipatikana lakini kila klabu iliambulia mgawo kiduchu wa Sh. milioni 11.1 tu.

Hali hiyo iliendelea pia katika mechi ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezwa Jumamosi Oktoba 20 kwenye Uwanja wa Taifa na kumalizika kwa wenyeji kushinda 3-2.

Licha ya mechi hiyo kuingiza Sh. milioni 47.6, Yanga na Shootings kila moja iliambulia mgawo kiduchu wa Sh. milioni 8.4.

Ni makato makubwa yanayozua maswali tele ambayo majibu yake hayajawahi kutolewa.

Kwa kutumia mfano wa mechi ya Simba dhidi ya Kagera Sugar, makato halisi yalikuwa kama ifuatavyo:

1. Maandalizi ya uwanja (pitch preparation) Sh. 400,000
2. Uwanja Sh. 3,671,261.85
3. Usafi na ulinzi wa uwanja Sh. 2,350,000
4. Ulinzi wa mechi Sh. 3,500,000
5. Gharama za mchezo Sh. 3,671,261.85
6. Umeme Sh. 300,000
7. Wachina (stadium technical support) Sh. 2,000,000
8. Tiketi ni Sh. 3,183,890.
9. Posho ya msimamizi wa kituo Sh. 120,000
10. Kamishna wa mechi Sh. 250,000
11. Waamuzi Sh. 440,000
12. Mwamuzi wa akiba Sh. 70,000
13. Mtathimini wa waamuzi Sh. 254,000
14. Kamati ya Ligi Sh. 3,671,261.85
15. Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) Sh. 2,202,757.11
16. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Sh. 1,468,504.74.
17. Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni Sh. 8,924,491.53.

Kwa mchanganuo huo inamaanisha kwamba zaidi ya Sh. milioni 36 zilimezwa katika makato wakati klabu ziliambulia jumla ya Sh. milioni 22.

Vilio vimekuwa vikubwa sasa kwa sababu ni makato mengi mno yanayoua timu zetu changa ambazo zinahitaji sapoti ya serikali, ambayo badala yake imekuwa ikizikamua.

Miongoni mwa makato yanayochefua ni ya "Uwanja", "Maandalizi ya Uwanja", "Usafi wa Uwanja na Ulinzi" na "Ulinzi wa mechi". Ni kwa vipi unaweza kumshawishi mtu kwamba hivyo ni vitu vinne tofauti?

Miongoni mwa maswali magumu ambayo hayajatolewa majibu ni haya:

UWANJA
Makato ya "Uwanja" peke yake, yanathibitisha kwamba uwanja huo unakodishwa, hivyo ili kuutumia ni lazima ulipie. Ndio maana Simba na Kagera Sugar wakatozwa Sh. milioni 3.6. Je, klabu zinaruhusiwa kuukodi kwa kulipa mapema kiasi hicho cha pesa na kisha waone wenyewe kama watahitaji kulipia umeme, kama watahitaji sapoti ya kiufundi kutoka kwa Wachina?

MAANDALIZI YA UWANJA
Malipo ya "Uwanja" yanatumika kufanya kazi gani ikiwa pia kuna malipo ya "Maandalizi ya Uwanja" na "Gharama za Mchezo"?
Tofauti ya malipo haya iko wapi? Je, makato ya 'Usafi wa Uwanja na Ulinzi" siyo "Maandalizi ya Uwanja"? Kwani mtu anaposema maandalizi ya uwanja huwa anamaanisha nini?

USAFI WA UWANJA NA ULINZI
Licha ya kuwapo kwa makato ya "Maandalizi ya Uwanja" pia kuna makato haya ya "Usafi wa Uwanja na Ulinzi". Je, wanapofanya usafi uwanjani hayo siyo maandalizi ya uwanja? Na kama usafi ni maandalizi ya uwanja, kwanini ni makato tofauti? Na "ulinzi" huu ni upi ambao kwa pamoja na usafi unagharimu jumla ya Sh. milioni Sh. 2,350,000 ilhali vyoo ni vichafu na unaweza hata kuzimia ukipita nje tu, acha kuingia ndani?

ULINZI WA MECHI
Licha ya kwamba makato ya ulinzi yameshakatwa katika kategori iliyopita ya "Usafi na Ulinzi", pia kuna makato mengine tofauti ya "Ulinzi" pekee ambayo yanagharimu Sh. milioni 3.5. Kama uwanja unalindwa na askari polisi ambao wanalipwa mishahara na serikali iliyowaajiri kwa ajili ya kulinda nchi, fedha hizi Sh. milioni 3.5 zinakwenda wapi?

GHARAMA ZA MCHEZO
Makato ya zilizopewa jina la "gharama za mchezo" katika mechi ya Simba dhidi ya Kagera Sugar zilikuwa Sh. milioni 3.67. Je, gharama za mchezo hazipaswi kujumuisha malipo ya waamuzi, ulinzi wa mechi, usafi na maandalizi ya uwanja? Kwanini haya yote ni makato tofauti? Au kinachohitajika ni lazima makato yawe mengi ili fungu kubwa likatwe tu?

UMEME
Kwa mfano umeme hulipiwa Sh. 300,000 katika takriban kila mechi ilhali mechi karibu zote huchezwa mchana? Fedha hizi zinazokatwa pengine mara tatu (Sh. 900,000) katika siku 8 zinaenda kulipia umeme upi? Wa Tanesco au wa jenereta? Ni kweli umeme wa kila saa 2 kwenye uwanja ule ni Sh. 300,000? Au klabu zinakamuliwa ili kulipia umeme wa hata siku ambazo hawautumii?

WACHINA
Wachina hawa wapo kutoa sapoti ya kiufundi. Je, anayepaswa kuwalipa ni mmiliki wa uwanja ama anayeukodi? Hii sapoti ya kiufundi inayogharimu Sh. milioni 2 (mara tatu Sh. milioni 6) ndani ya siku 8 ni ipi? Wanatoa sapoti gani ya kiufundi katika mechi hizi zinazochezwa mchana kweupe? Ikiwa mechi zenyewe hazirushwi na kituo chochote cha TV na hata wakirusha hawatumii chumba (control room) cha uwanja wanatumia magari yao ya 'van', ni sapoti gani wanayotoa Wachina hawa?

Makato ya Wachina yanashangaza, kwasababu wao ndiyo waliojenga uwanja kwa pesa ya msaada wa nchi yao na pia Serikali ya Tanzania. Sasa cha kujiuliza ni kwamba uwanja ule bado uko mikononi mwao?

Je, walipomaliza kujenga uwanja hawakuukabidhi kwa Watanzania na badala yake wakaingia ubia kuumiliki?

Ina maana Uwanja wa Taifa unamilikiwa na Wachina kwa upande mmoja na Serikali kwa upande mwingine ndiyo maana kila mmoja anakuwa na makato yake?

VAT
Makato ya ongezeko la thamani (VAT) katika mechi hii ya Simba dhidi ya Kagera Sugar yalikuwa Sh.8,924,491.53. Kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria za kodi hapa. Ikiwa pia kuna makato ya umeme, ambapo kwenye umeme pia huwa kuna VAT, je, ni sahihi kulipa VAT mara mbili katika 'bidhaa' (mechi) moja?

DRFA
Lakini pia haya makato ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam DRFA ni ya nini na yanakwenda kufanyia kazi gani ikiwa kwa sasa vyama vya soka vya wilaya za Dar es Salaam (KIFA - Kinondoni, TEFA - Temeke na IDFA - Ilala) vyote vimeshapewa hadhi ya mikoa na vinaendesha ligi zao?

Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser alisema makato hayo yanawaumiza na kuwakwaza kiuchumi, hivyo akazitaka klabu kuungana ili kulipatia ufumbuzi suala hilo ambalo limekuwa tatizo kubwa kwa maendeleo ya klabu za soka nchini.

Naye meneja wa Azam, Patrick Kahemele anazigeukia klabu kuwa zenyewe ndizo zinapaswa kujilaumu kwa kuipa madaraka makubwa TFF katika kupanga gharama za tiketi, kiingilio na makato mengine ya gharama za mechi husika, hali ambayo mwishowe huwaacha wakiambulia fedha kidogo mno kutokana na mapato ya milangoni.

“Haya yote yanatokea kwa sababu mwanzo wetu haukuwa mzuri. Klabu hazina umoja. Kama tungeungana katika hili, kusingekuwa na malalamiko,” alisema Kahemele na anaongeza.

“Vitabu vya tiketi za uwanjani viko TFF na klabu hazioneshwi, kuna gharama za waamuzi, ulinzi, gharama za mchezo, maandalizi ya uwanja, gharama za mchezo, pesa ya Kamati ya Ligi. Katika hali kama hii tunategemea klabu itanufaika na kiingilio cha mechi."

Mmoja wa wamiliki wa klabu ya African Lyon, Rahim Kangezi naye anasema wamekuwa wakisikitishwa na hali ya makato inayofanywa na TFF na serikali dhidi ya klabu za Ligi Kuu.

Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga anasema klabu yao pia imekuwa ikiathiriwa na makato makubwa.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari hivi karibuni, Rais wa TFF, Leodgar Tenga alisema kuwa makato yote katika kila mechi yanafuata sheria na taratibu zilizopo.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema asilimia 60 ya makato yote inakwenda serikalini na kwamba pia wanalazimika kutoa fedha Sh. 200,000 kwa ajili ya mafuta ya magari ya polisi.

Simba na Yanga ziliwahi kutishia kutocheza tena kwenye Uwanja wa Taifa kuepuka makato makubwa misimu kadhaa iliyopita na Serikali iliwapoza kwa kuahidi kushughulikia suala hilo.

Hata hivyo, inaonekana hakuna juhudi za kulishughulikia suala hilo hivi karibuni, licha ya Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Sethi Kamuhanda, kuiambia NIPASHE hivi karibuni kwamba wanaweza kukaa chini kuliongelea jambo hilo.
Lakini pamoja na hayo, kinachoonekana hapa bila klabu kuunganisha nguvu na kupinga hili hakuna chochote kitakachofanyika.

Chanzo: Gazeti la NIPASHE la Oktoba 23, 2012.

No comments:

Post a Comment