Wednesday, October 10, 2012

IKER CASILLAS: NITAMCHAGUA CRISTIANO RONALDO TUZO YA MWANASOKA BORA WA DUNIA NA SIYO MESSI WA BARCA

Iker Casillas (kulia) na Cristiano Ronaldo
Kipa Iker Casillas (kushoto) na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid wakiwapungia mikono mashabiki wa klabu yao mjini Plaza de Cibeles jijini Madrid, Mei 3, 2012 baada ya kutwaa ubingwa wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania.
MADRID, Hispania
Nahodha wa Real Madrid, Iker Casillas amesema atamchagua mchezaji mwenzake Cristiano Ronaldo katika kura ya kuchagua mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia na siyo Lionel Messi wa mahasimu wao wa jadi, Barcelona.

Mastraika wote hao wawili walifunga mabao yote ya timu zao katika mechi ya 'El Clasico' baina yao iliyochezwa Jumapili.

Casillas amesema: "Nitamchagua Cristiano, hili liko wazi, ni kwa sababu yeye ni mchezaji anayetupa mambo mengi na amekuwa akitupa mafanikio katika misimu michache iliyopita na pia ni mchezaji ambaye nimekuwa naye kila siku. Namjua, namjua yukoje, najua anavyojifua, najua anataka nini, najua anataka kushinda nini na kwakweli amekuwa akifanya kila analoweza kwa ajili yetu."


Wiki chache zilizopita, Casillas alikuwa akijiumauma kila mara alipoulizwa ni nani kati ya Messi na Ronaldo atakayempigia kura ashinde tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia.

VITA YA UBINGWA
Casillas amesisitiza kwamba La Liga, Ligi Kuu ya Hispania bado haijafikia mwisho baada ya kutoka sare ya 2-2 dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Barcelona.

Matokeo hayo katika mechi ya Jumapili yameiacha Real Madrid katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi lakini Casillas haamini kwamba hatua iliyofikiwa sasa ni mwafaka kutabiri mambo mengi kuhusiana na ligi hiyo.

"Kama bado tutakuwa nyuma kwa pointi nane hadi kufikia Desemba, hapo ninaweza kuingiwa na hofu kuhusiana na La Liga," amesema kipa huyo ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Hispania.

"Lakini sasa, bado kuna mechi nyingi za kucheza. Sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa Camp Nou ni matokeo mazuri, hata kwa kuangalia wastani wa mabao."

No comments:

Post a Comment