Saturday, October 27, 2012

GARETH BALE AFUKUZIWA KWA DAU NONO REAL MADRID, MOURINHO AANZA MISHEMISHE ZA KUMNG'OA TOTTENHAM

Gareth Bale
LONDON, England
Kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho ameripotiwa kuwa yuko 'bize' kuhakikisha kwamba anaimarisha kikosi chake kwa kumsajili winga nyota wa klabu ya Tottenham, Gareth Bale

Gazeti la Hispania la AS limefichua katika taarifa yake ya leo kwamba Real wanamtaka sana winga huyo anayechezea pia timu ya taifa ya Wales na kwamba, ndiye mchezaji namba moja waliyepania kumtwaa wakati wa kipindi kijacho cha usajili, huku pia taarifa zilizoripotiwa leo na gazeti la Mirror la Uingereza zikidai kuwa Mourinho amekutana na rais wa Real Madrid, Florentino Perez na kumshawishi atume ofa rasmi ya kumtwaa Bale.

Bale, 23, hivi karibuni alisaini mkataba mpya wa kuichezea Tottenham kwa muda mrefu hadi mwaka 2016, lakini Real hata hivyo wako tayari kumtwaa kwa gharama yoyote.

Mourinho anaonekana kupania kuongeza makali katika safu yake ya ushambuliaji baada ya Real Madrid kuanza msimu huu kwa kusuasua, huku wakionekana kutofanya vizuri katika La Liga, Ligi Kuu ya Hispania na pia katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Real ilisaini mkataba wa kirafiki na Tottenham baada ya kumnunua Luka Modric kutoka katika klabu hiyo wakati wa usajili uliopita wa majira ya kiangazi na urafiki huo utakuwa muhimu zaidi kama mpango wa kuuziana Bale utakamilika.

Huku uhamisho wa Bale ukitarajiwa kuzidi thamani ya paundi za England milioni 50 (Sh. bil 130), Mourinho anaweza kulazimika kuwauza baadhi ya nyota wake wa sasa ili kujiongezea fedha, huku Kaka na Mesut Ozil wakitajwa kuwa miongoni mwa nyota wanaoweza kuondoka Bernabeu.

Hivi sasa Bale yuko nje ya kikosi cha Tottenham baada ya kuruhusiwa kwenda katika likizo ya uzazi kufuatia mkewe kujifungua mtoto wao wa kwanza Jumamosi iliyopita.

No comments:

Post a Comment