Tuesday, October 16, 2012

FIFA KUIJAZA MIHELA REAL MADRID BAADA YA BEKI WAKE MARCELO KUUMIA AKIWA TIMU YA TAIFA YA BRAZIL… NI KUPITIA SHERIA MPYA YA FIDIA KWA KLABU ILIYOANZA MEI


Marcelo anavyoonekana na 'hogo' lake leo (Oktoba 16, 2012) baada ya kuvunjika mfupa wa mguu akiwa mazoezini na timu ya taifa lake la Brazil.
MADRID, Hispania
FIFA italipa mshahara wa Marcelo katika kipindi chote atakachokuwa nje kutokana na majeraha kupitia sheria mpya inayozilinda klabu, ambayo imeanza kutumika rasmi Mei mwaka huu.

Katika mpango huo wa bima, FIFA itakuwa ikizilipa fidia klabu ambazo wachezaji wake wataumia wakati wakizitumikia timu za mataifa yao wakati wa michuano ya kimataifa.

Klabu ambazo zitashindwa kuwatumia wachezaji wake kwa siku 28 mfululizo au zaidi kutokana na majeraha, kama ilivyo kwa Marcelo atakayekosekana Real Madrid kwa miezi mitatu, zitakuwa na haki ya kudai fidia kupitia mpango huo, ambao unatoa fidia ya juu kwa siku kuwa ni euro 20,548 (Sh. milioni 40). Kiwango hiki cha ukomo kimewekwa kwa kuzingatia bajeti yote ya jumla ya mpangp huo ambayo ni euro milioni 60 (Sh. bilioni 120).

Kiwango cha fidia huzingatia mshahara wa mchezaji katika klabu yake kama mfanyakazi, hii ikimaanisha kuwa ni pamoja na kiwango anacholipwa kwa wiki au kwa mwezi, pamoja na malipo yote ya huduma za kijamii.

Kwa kuzingatia kwamba Marcelo hulipwa euro milioni 2.3 (Sh. bilioni 4.6) kwa mwaka baada ya kukatwa kodi, FIFA italazimika kuilipa Real Madrid euro 6,300 kwa siku (Sh. milioni 12.7) hadi beki huyo wa kushoto atakapopona na kurejea uwanjani kwa ruhusa ya madaktari.

Hivi sasa Real Madrid bado wanasubiri kujua ni kwa muda gani beki huyo wa kimataifa wa Brazil atakuwa nje baada ya kuumia wakati akiwa mazoezini.

Wakilipwa na FIFA kwa miezi mitatu ya kuwa nje kwa Marcelo kama inavyotazamiwa,  Real Madrid wataingiza fedha za ziada kupitia mpango huo kiasi cha euro 574,000 (Sh. bilioni 1.2).
 

No comments:

Post a Comment