Tuesday, October 2, 2012

Bilioni 280 kusaidia usambazaji wa mji katika jiji la Dar na Chalinze


Na Tiganya Vincent-MAELEZO-Dar es salaam
SERIKALI ya India kupitia Benki ya EXIM imeikopesha Tanzania Sh. bilioni 280 kwa ajili ya usambazaji maji katika Jiji la Dar es salaam na mji wa Chalinze mkoani Pwani.

Mkopo huo umesainiwa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Fedha Dr. William Mgimwa kwa upande wa Tanzania na Meneja Mkuu wa Benki ya EXIM ya India Bibi Geeta Poojary.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkopo huo Waziri wa Fedha alisema kuwa mkopo huo umekuja kwa wakati ili kuisaidia Tanzania kukabiliana na uhaba wa maji katika jiji la Dar es salaam na maeneo ya Chalinze mkoani Pwani.

Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuboresha huduma za jamiii na kiuchumi kwa wakazi wa maeneo husika badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji badala yake wautumie katika kujiongezea kipato na kukabiliana na umasikini.

Dkt. Mgimwa alisema kuwa mradi huo utasaidia kuongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo milioni 82 hadi kufikia mita za ujazo milioni 196 kwa siku.

Aliongeza kuwa pia mradi huo utahusisha ujenzi wa njia ya usafirishaji wa maji na kuongeza mtandao wa usambazaji kwa wateja.

Dkt. Mgimwa aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo itakuwa sehemu ya kutekeleza Mkakati wa Kukuza Uchumi na kupunguza Umaskini(MKUKUTA) na kupunguza magonjwa yatokana na maji yasiyokuwa salama.

Alisema kuwa Tanzania itatakiwa kulipa  mkopo huo kwa kipindi cha miaka ishirini (20) ambapo kabla ya kuanza kulipa Tanzania itakuwa  miaka mitano ya unafuu (grace period) kabla ya kuanza malipo.

Dkt. Mgimwa aliongeza kuwa mkopo huo ni moja ya mikopo nafuu sana kwani Tanzania itatakiwa kulipa riba ya asilimia  1.75 ya mkopo .

No comments:

Post a Comment