Tuesday, October 16, 2012

BARCELONA, REAL MADRID ZAWEKA BIFU KANDO... ZASHIRIKIANA KUKODI NDEGE YA KUWASAFIRISHA LIONEL MESSI, DI MARIA, JAVIER MASCHERANO, GONZALO HIGUAIN NA ALEXIS SANCHEZ BAADA YA ARGENTINA VS CHILE ..!

Messi, Higuain na Di Maria
Messi na Mascherano wakiwa katika mazoezi ya timu yao ya Argentina

Sanchez akiitumikia timu yake ya taifa ya Chile.


BUENOS AIRES, Argentina
Real Madrid na Barcelona zimekubaliana kushirikiana katika kujichangisha fedha za kukodi ndege binafsi ya kuwarejesha Hispania wachezaji wao kutoka mjini Santiago de Chile mara tu baada ya kumalizika kwa mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia kati ya Chile na Argentina itakayochezwa leo Jumanne (Oktoba 16, 2012).

Itakapomalizika tu mechi hiyo, wachezaji wa Real Madrid ambao ni Gonzalo Higuaín na Di María, na wale wa Barcelona ambao ni Lionel Messi, Javier Mascherano na Alexis Sánchez, na kocha wa viungo wa Barcelona, Juanjo Brau, watapanda ndege moja itakayosafiri kwa saa 15 kuwafikisha katika jiji la Madrid. Wachezaji wa Barça wataendelea na safari hiyo hadi mjini Barcelona.

Ndege hiyo ya kukodi itatua Hispania kesho Jumatano mchana. Kwa sababu ya kutumia usafiri huo, wachezaji hao watapata muda wa kupumzika wa zaidi ya siku moja na nusu.

Katika hali ya kawaida, ndege za kawaida za kusafirisha abiria huwa hazitui hadi keshokutwa (Alhamisi) mchana, na hilo lingemaanisha kuwa nyota hao wasingeweza kujifua na wenzao kabla ya mechi zao za Jumamosi katika La Liga, Ligi Kuu ya Hispania. Real Madrid watawakribisha Celta na Barça watakuwa ugenini kucheza dhidi ya Coruña.

Mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo nchini Chile, abiria hao sita watasafirishwa hadi kwenye Uwanja wa Ndege wa Santiago. Kuna umbali wa takriban kilomita 10,000 kati ya mji mkuu wa Chile na wa Madrid nchini Hispania. Gharama za kukodi ndege hiyo binafsi ni dola za Marekani 200,000 (Sh. milioni 310), ambazo zitalipwa kwa pamoja na Real Madrid na Barcelona.

No comments:

Post a Comment