Sunday, October 21, 2012

25 SERENGETI BOYS WAINGIA KAMBINI


KIKOSI cha wachezaji 25 wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kimeingia kambini leo (Oktoba 21 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya raundi ya mwisho ya michuano ya Afrika kwa vijana.

Serengeti Boys ambayo iko chini ya Kocha Jakob Michelsen itacheza mechi hiyo ya raundi ya tatu na mshindi kati ya Congo Brazzaville na Zimbabwe ambapo tayari Congo Brazzaville imefanikiwa kupata ushindi wa ugenini wa mabao 2-1. Mechi ya marudiano itachezwa jijini Brazzaville kati ya Oktoba 26-28 mwaka huu.

Katika mechi hiyo ya raundi ya tatu, Serengeti Boys itaanzia nyumbani katika mchezo utakaofanyika Novemba 17 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, wakati mechi ya marudiano itachezwa wiki mbili baadaye.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liko katika mikakati ya kuhakikisha Serengeti Boys inapata mechi mbili za kirafiki za kimataifa kabla ya kumvaa mshindi kati ya Congo Brazzaville na Zimbabwe. Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitafanyika Machi mwakani nchini Morocco.

No comments:

Post a Comment