Sunday, September 23, 2012

XAVI AFUNGA 'GOLI LA USIKU' BARCA IKIIPITA REAL MADRID KWA POINTI 11

Xavi Hernandez (wa pili kushoto) akishangilia pamoja na wachezaji wenzake goli lake alilofunga dhidi ya Granada wakati wa mechi yao ya La Liga usiku kuamkia leo kwenye Uwanja wa Nou Camp, mjini Barcelona.
Lionel Messi wa Barcelona (kushoto) akishangilia na wachezaji wenzake Christian Tello na Xavi Hernandez baada ya kufunga goli lao la pili dhidi ya Granada wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Hispania kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona jana Septemba 22, 2012. Beki wa Granada alijifunga kufuatia krosi ya Messi. Barcelona walishinda 2-0.

BARCELONA ilifunga magoli ya dakika za lala salama na kuilaza Granada 2-0 jana usiku.

Goli kali la dakika ya 87 kutoka kwa mtokea benchi Xavi lilibomoa "basi gumu lililoegeshwa" langoni mwa Granada katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Hispania kwenye Uwanja wa Nou Camp.

Xavi, ambaye aliingia katika dakika ya 53 kuchukua nafasi ya Thiago Alcantara, hatimaye aliweza kuuzidi ujanja ukuta madhubuti wa wageni kwa goli kali la shuti la nje ya boksi lililogonga besela na kutinga wavuni.

Ilikuwa ni mechi ngumu kwa Granada pia, ambao kipa wao Tono aliokoa mashuti mengi kwa ufundi wa hali ya juu, na kuteleza kwao kukakamilika wakati Borja Gomez alipojifunga mwenyewe kufuatia krosi ya hatari kutoka kwa Lionel Messi.

Ulikuwa ni ushindi wa tano katika mechi tano mfululizo kwenye La Liga na kuwafanya Barca kuwaacha mahasimu wao Real Mardid kwa pointi 11, kabla ya mabingwa wenye pointi 4 kucheza mechi yao ya tano leo usiku ugenini kwa Rayo Valecano.

Kocha Jose Mourinho ambaye alisema "sina timu" kufuatia kipigo kutoka kwa Valencia, amesema timu yake imebadilika baada ya ushindi wa 3-2 dhidi ya Manchester City katika mechi yao ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

No comments:

Post a Comment