Saturday, September 22, 2012

WENGER: TUNAWEZA KUMUUZA WALCOTT JANUARI

Theo Walcott wa Arsenal akikokota mpira wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Southampton kwenye Uwanja wa Emirates mjini London, Septemba 15, 2012. Arsenal ilishinda 6-1 na Walcott 'alitupia' moja.

KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema hawezi kufuta uwezekano wa kumuuza Theo Walcott Januari.

Mkataba wa sasa wa Walcott unamalizika Juni.

Wenger atafikiria kumuuza Walcott — anayetakiwa na Chelsea na Liverpool — katika kipindi cha usajili kijacho.

Alikiri: "Itategemea mahitaji ya timu na klabu. Tunaweza kuvumilia akae hadi mwisho wa mkataba wake kama itahitajika.

"Hebu tutumai kuwa tutapa suluhisho ndani ya miezi miwili ijayo.

"Hakuna mchezaji anayekuwa na furaha anapokuwa hachezi."

Alisema watajitahidi kuona anasaini mkataba mpya kabla ya Desemba.

Kama hatasaini, Walcott atakuwa huru kuzungumza na klabu anayoitaka Januari na akaondoka bure mwisho wa msimu.

Wenger alisema: "Kadri suala linavyochukua muda kumalizika ndivyo linavyozidi kuwa gumu. Bado nina matumaini ya kumpa mkataba mpya na miezi miwili ijayo ni muhimu sana."

Winga huyo wa timu ya taifa ya England, ambaye hajaanza katika mechi hata moja tangu mazungumzo ya mkataba wake mpya yalipovunjika, amekataa ofa ya Arsenal ya mshahara wa paundi 75,000 kwa wiki. Hivi sasa analipwa paundi 55,000 kwa wiki na anataka mshahara wa paundi 100,000 kwa wiki.

No comments:

Post a Comment